USHIRIKI wa wananchi katika ulinzi shirikishi kupitia Polisi Jamii umeleta mafanikio katika kupunguza vitendo vya uhalifu nchini. Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyihaji Makame wakati akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mpangokazi Idara ya Uratibu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika Ofisi hiyo.
Dk. Mwinyihaji amesema katika kuimarisha ulinzi na usalama jumla ya vikao 58 vya Kamati za Ulinzi na Usalama vimefanyika Unguja na Pemba lengo likiwa ni kuimarisha ulinzi na kuhamasisha wananchi kushiriki zaidi katika ulinzi wao wenyewe na mali zao.
Kuhusu suala la mifugo inayozurura ovyo mijini kwa kuanzia amesema operasheni maalum inaendelea katika Manispaa ya Zanzibar ambapo Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Baraza la Manispaa hadi sasa wameshakamata mifugo 153 iliyokutwa ikizurura ovyo.
Kati ya mifugo hiyo alieleza ng’ombe 43, mbuzi 58 na punda mmoja wameshakombolewa na Serikali imekusanya jumla ya shilingi milioni 4.3 ikiwa ni faini kutoka kwa wamiliki wake. Katika taarifa yake Waziri Mwinyihaji ameeleza kazi ya kuung’arisha mji wa Zanzibar inaendelea ambapo mradi wa majaribio kwa kuweka taa za barabarani kwa kutumia umeme jua umeanza majaribio ambapo taa katika baadhi ya mitaa ya Manispaa zimeanza kuwashwa.
Waziri aliongeza kuwa Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa zinaendelea kuimarisha utoaji huduma mbalimbali kwa wananchi kwa kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali zikiwemo afya, maji, elimu
na huduma za kiuchumi na biashara kama vile ujenzi na ukarabati wa masoko na huduma zake kama sehemu za kufanyia biashara na vyoo.
Kikao hicho cha tathmini ya Mpangokazi ambacho kiko chini ya uenyekiti wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kimehudhuriwa pia na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharrif Hamad na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.