Ulimboka apelekwa A. Kusini

DK. Steven Ulimboka

Hatimaye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka amesafirishwa jana, kwenda nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi baada ya baadhi ya vipimo kukosekana nchini.

Dk. Ulimboka alisafirishwa jana kwa ndege ambayo haikuwekwa bayana ni ya shirika gani iliyoondoka saa 10:30 jioni kwenye uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere, chini ya ulinzi mkali wa madaktari .

Atakapowasili kwenye hospitali aliyopangiwa, miongoni mwa vipimo atakavyofanyiwa ni “Toxicology” ambacho hutumika kuangalia sumu mwilini.

Dk. Ulimboka aliondoka jana saa 6:15 mchana kutoka wodi ya Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) na gari la kubeba wagonjwa la hospitali binafsi ya AAR lenye namba za usajili T 151 AVD na kupelekwa kwenye jengo la watoto lililopo Muhimbili kwa ajili ya kuwekewa mashine ya ‘Dialisis’ ambayo hutoa ama kuchuja taka/sumu mwilini. Kwa kawaida kazi hii hufanywa na figo.

Wakati anaondolewa wodini na kuingizwa kwenye gari hilo, milango mikuu ya kuingilia Moi ilifungwa na kutoruhusu mtu yeyote isipokuwa madaktari.

Pamoja na kuwepo kwa mazingira ya kulinda usalama wa Dk. Ulimboka dhidi ya wabaya wake, waandishi wa habari waliokuwa wamekaa nje ya lango hilo baada ya kuzuiwa kuingia walifanikiwa kupiga picha gari la wagonjwa bila kujua kama ndilo lililombeba au la.

Dakika kumi baada ya gari hilo kutoka, jopo la madaktari waliokuwa wakimshughulikia lilitoka bila kuzungumza chochote na waandishi na kuelekea eneo lililopo jengo la kuhifadhia maiti ndani ya hospitali hiyo.

Kutokana na hali hiyo waandishi wa habari waliendelea kukaa eneo hilo huku wakiwa wametegesha kamera zao wakisubiri mgonjwa huyo atolewe kutoka kwenye gari huku gari lingine la wagonjwa kubaki ndani ya jengo hilo.

Lakini daktari mmoja alifika hapo na kuwataarifu waandishi kuwa, tayari mgonjwa ameshatolewa na wakati huo alikuwa jengo la watoto kwa ajili ya kuwekewa mashine hiyo kwa ajili ya kuanza safari ya kuelekea Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere kwa safari.

Hata hivyo, magari ya waandishi wa habari, ndugu wa Dk Ulimboka pamoja na costa mbili za madaktari zilizokuwa zimekodishwa kwa ajili ya kumsindikiza mwenzao uwanja wa ndege, yalikwama kwenye foleni kubwa iliyokuwa barabara ya Mandela na kusababisha kukaa hapo kwa muda wa saa nzima na kushindwa kumuona daktari huyo wakati akiondoka.

Kutokana na hali hiyo, madaktari hao waliungana na wanaharakati waliokuwa wamefika eneo hilo kubeba mabango yaliyokuwa na ujumbe tofauti kwa serikali na kuanza kuimba nyimbo zilizokuwa na ujumbe wa kuunga mkono juhudi za Dk. Ulimboka.

Wanaharakati hao ni pamoja na Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake nchini (Tamwa), Ananilea Nkya na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu, Dk Hellen Kidjo -Bisimba.

Baadhi ya mabango hayo yalisomeka “Serikali kama Muhimbili kungekuwa na dawa Dk. Ulimboka angetibiwa na madaktari wenzake”.

“Madaktari wamegoma kwa sababu hospitali za serikali hazina vitendea kazi, wananchi wanapoteza maisha bila huruma”.

“Rais Kikwete ahadi yako ya mgomo wa madaktari kuwa historia hapa Tanzania imeishia wapi tekeleza ahadi yako”, “Hata mkituua utetezi utaendelea”, “bilioni 200 za kuagiza madaktari nje ya nchi zinatosha kuboresha huduma za afya na kumaliza mgomo wa madaktari” na “Tunadai bajeti ya afya ifikie asilimia 15 kama utekelezaji wa azimio la Abuja”.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Katibu wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Edwin Chitage, alisema kwamba sababu kubwa ya kumpeleka mgonjwa wao nje ya nchi imetokana na vipimo anavyotakiwa kufanyiwa kukosekana nchini.

Aliongeza kuwa, hali ya Dk. Ulimbona ilibadilika toka juzi na kwamba, figo zake hazifanyi kazi vizuri.

“Kuna aina ya vipimo anatapaswa kufanyiwa na hospitali zetu zote hazina vipimo hivyo, kwa kweli mwenzetu yupo katika hali mbaya anaumwa sana, kundi aliloondoka nalo leo ni pamoja na madaktari bingwa,” alisema.

Kuhusu nini kinafuata baada ya mwenzao kwenda nje kwa matibabu, Dk. Chitage alisema kuwa, wakati wowote kuanzia sasa watatoa tamko lao na kueleza kuwa mgomo bado unaendelea.

Aliitaka serikali itoe tamko dhidi ya hofu waliyonayo kuhusu maisha ya madaktari hasa kutokana na unyama aliofanyiwa mwenzao.

Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja nchi anayopelekwa Dk. Ulimboka na kueleza kuwa, familia yake ndiyo itakayoeleza hilo ambapo hata ndugu zake walipoulizwa hawakuwa tayari kuitaja kwa madai kuwa ni kwa ajili ya usalama wa ndugu yao.

Alishukuru mwitikio mkubwa wa watu waliojitokeza kutoa michango yao ili kumwezesha mwenzao kwenda nje ya nchi na kueleza kuwa, taarifa za fedha hizo zitatolewa ili kuwepo na uwazi.

Miongoni mwa waliofika asubuhi kumjulia hali Dk. Ulimboka kabla ya kusafirishwa ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mkama na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa.

HOSPITALI DAR HALI BADO TETE

Nipashe Jumapili ilizungukia baadhi ya hospitali binafsi ilikuta hali ni tete baada ya kuelemewa na wagonjwa na nyingine kushindwa kuwapokea.

Hospitali ambazo zimeshindwa kupokea wagonjwa ni pamoja na Hindu Mandal huku Imtu idadi ya wagonjwa ikiwa ni kubwa kuliko uwezo wao.

Hospitali ya Aga Khan, Ocean Road kwa upande wao wanaendelea kupokea wagonjwa huku hospitali za serikali Muhimbili, Moi, Amana, Temeke na Mwananyamala hali ya mgomo inaendelea.

WANAHARAKATI

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Nkya amewataka Watanzania kwa umoja wao waungane kulaani kitendo hicho alichofanyiwa Dk. Ulimboka.

Alisema haiwezekani kuzima sauti za wananchi kwa kuwaua kinyama. Pia ameitaka serikali itambue kuwa, kama Muhimbili kungekuwa na vifaa, Dk. Ulimboka angetibiwa na wenzake hapa nchini.

Kadhalika alionyesha kushangazwa na kitendo cha serikali kwa mwaka jana kutumia kiasi cha Sh. bilioni 5 kwa ajili ya matibabu ya viongozi nje ya nchi na kueleza kuwa, fedha hizo zingetumika kununulia vifaa hospitali za hapa nchini.

KCMC YATIMUA MADAKTARI 80

Madaktari zaidi ya 80 waliokuwa wanafanya mazoezi ya vitendo katika hospitali ya Rufaa ya KCMC wamefukuzwa kazi na kupewa saa 24, kukabidhi mali zote za hospitali.

Katika barua hiyo ya Juni 29, mwaka huu, kwenda kwa madaktari hao, iliyosainiwa na Menejimenti ya hospitali hiyo, madaktari hao walipewa muda wa kuanzia saa 9 alasiri hadi saa 8 mchana wa Juni 30, mwaka huu, wawe wameondoka.

Wakizungumza na NIPASHE, baadhi ya madaktari walisema kuwa serikali ilitoa vitisho kuwa kama hawataondoka muda uliotakiwa polisi wangetumika kuwaondoa.

Aidha, baadhi ya madaktari ambao wapo kwenye masomo ya Uzamili na Uzamivu, wamesema wao wanaendelea na masomo kama kawaida, lakini hawatafanya kazi kwani kazi ni lazima waigomee kwa kuwa madai wanayodai ni ya msingi na yenye manufaa kwa Watanzania wote.

Kutokana na mgomo huo hali ya utoaji huduma imeendelea kudhorota, huku wengi wakiendelea kukosa huduma.

BUGANDO: 47 WAPEWA BARUA WAANDISHI “NO” KURIPOTI

Wakati kukiwa na taarifa kwamba madaktari bingwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza wanajiandaa na mgomo uongozi wa hospitali hiyo umepiga marufuku waandishi wa habari kwenda kupata taarifa za mgomo wa madaktari unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Madaktari hao bingwa wanadaiwa kutangaza mgomo kutokana na kuzidiwa majukumu ya kuhudumia wagonjwa baada ya wenzao kuwa katika siku ya saba tangu walipoanza mgomo kuishinikiza serikali kutekeleza madai yao mbalimbali ikiwemo kuboreshewa maslahi na vifaa tiba vya kutosha.

Hata hivyo, mwandishi wa gazeti hili alipofika hospitalini hapo jana kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa taarifa za madaktari bingwa kukusudia kugoma, alizuiwa na walinzi ambao walidai wamepata maelekezo kutoka kwa Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk. Charles Majinge, kwamba waandishi wa habari hawaruhusiwi kuingia kwa sababu hakuna taarifa za kuandika.

Wakati huo huo baadhi ya madaktari walio katika mafunzo ya vitendo jana walianza kukabidhiwa barua za kutimuliwa hospitalini hapo huku wengine wakigoma kuzipokea. Jumla ya madaktari 47 imedaiwa wameandikiwa barua za kufukuzwa kazi.

Ripoti hii imeandaliwa na Romana Mallya, Beatrice Shayo, Dar es Salaam, George Ramadhan, Mwanza na Salome Kitomari, Moshi

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI