Ukimwi waua watu mil 30, idadi hiyo pia waishi na VVU

UMOJA wa Mataifa (UN) unaeleza kwamba tangu ugonjwa wa Ukimwi ugunduliwe mwaka 1981, unakadiria kuuwa watu milioni 30, huku idadi kama hiyo ikiwa ndio wanaoishi na virusi vya HIV.

Hata hivyo ripoti ya hivi karibuni ya UN inaeleza licha ya kwamba idadi ya watu wanaoambukizwa Ukimwi kupungua kwa sasa katika nchi kadha, lakini bado mamilioni ya wagonjwa hawapati dawa stahili.

Madaktari wanasema virusi vya HIV sasa vinafahamika vizuri tofauti na ilivyokuwa hapo awali, na wagonjwa wanaofululiza kutumia dawa ya kupunguza makali ya Ukimwi kwa wakati wanaweza kuishi karibu maisha ya kawaida.

Mwaka wa 1981, daktari mmoja kutoka California, Marekani aliwabaini vijana wa kiume watano, walioshiriki katika mapenzi ya jinsia moja, wakiwa na ugonjwa usiokuwa wa kawaida. Walikuwa na homa ya pneumonia na saratani ya ngozi.

Dk. Gottlieb hakujua kuwa ripoti zake, ndio itakayokuwa historia ya kwanza kuandikwa juu ya ugonjwa ambao baadae ulikuja kuwa janga kubwa la mataifa mbalimbali (AIDS) au UKIMWI. Virusi vya HIV viligundulikana miaka miwili baada ya ugunduzi huo wa Dk. Gottlieb.

Tena damu ikaweza kupimwa kama ina virusi vya HIV, na baadae zikapatikana dawa kadha za kudhibiti ugonjwa huo.