UKAWA Wamtangaza Mgombea Wao, Asema Watashinda Kweupeee…!

Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa

Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa


UMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) unaoundwa na ushirikiano wa vyama vya CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD hatimaye umefikia mwafana na kumsimamisha mgombea mmoja wa urais na makamu wake kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA ambaye ataungwa mkono na vyama vyote.

Ni aliyekuwa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa na kada wa Chama Cha Mapinduzi aliyetangaza kukihama chama hicho mapema baada ya kudai kutendewa visivyo katika mchakato wa kumteuwa mgombea wa nafasi ya urais kupitia CCM. Lowassa ambaye sasa ni CHADEMA damu anaungana na mgombea mwenza, Juma Haji Duni aliyekihama chama cha wananchi, CUF ili aweze kutimiza makubaliano ya UKAWA ya kusimamisha mgombea mmoja katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka 2015.

Juma Haji Duni kapoteza nafasi yake ya Uwaziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na kupoteza nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha CUF na kujiunga na CHADEMA ili agombee pamoja na mgombea urais wa tiketi ya chama hicho.

Haji Duni anaungana na Lowassa na kupeperusha bendera ya CHADEMA kugombea urais huku wakiwa na kivuli cha mwamvuli wa UKAWA. Vyama vyote vimekubali kuwanadi wagombea hao kwa pamoja na pia kuachiana nafasi za ubunge na udiwani pia kwa kushirikiana. Kwa mantiki hiyo UKAWA itasimamisha mgombea mgombea mmoja wa ubunge na udiwani Tanzania Bara na Visiwani ili kujenga nguvu ya kukiangusha Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Chadema, ambapo ulitumika kuwatangaza wagombea hao, Lowassa alisema anaupokea mzigo mkubwa aliobebeshwa na UKAWA wa kugombea kwa mwamvuli wa vyama vyote na kudai yupo tayari kuubeba.

“…Naupokea mzigo huu kwa unyenyekevu mkubwa na kwa shukrani kubwa mzigo huu, asanteni sana kwa kuniamini imani uzaa imani, nataka niwaambie jambo moja namuomba mwenyezi mungu aendelee kunijalia afya njema anaiwezeshe kujibu shukrani na mapenzi mlionionesha kwa mapendo,” alisema Edward Lowassa.

Alisema anaomba Watanzania na wanachama wamuelewe kwamba hakuja kwa ajali CHADEMA bali alifikiri na kushauriana na familia na marafiki zake kisha akaridhika kuja CHADEMA. Alisema kazi ya chama cha siasa duniani ni kushika dola na CHADEMA imejiandaa kushika dola niwajibu wa kutala dola sasa hivi.

“…Nataka kuwaondoa wasiwasi Watanzania wanaohoji labda hiki ni chama kidogo hakiwezi kuongoza hapana TANU ilipewa madaraka ikiwa na miaka saba lakini nyinyi (CHADEMA) mna miaka 23, mmekijenga chama vizuri kina demokrasia mungu awape nini,” alisema Lowassa.

Alisema maamuzi magumu lazima yafanyike sasa hivi ili mambo yaende, alisema katika muungano wa UKAWA chama cha Chadema kimekuwa na nguvu kubwa hivyo kuna kila sababu ya kushinda uchaguzi mkuu. Alisema sasa ameanzisha safari ya mabadiliko nje ya CCM. “…Safari ya mabadiliko nje ya CCM, sfari ya mabadiliko nje ya CCM…watatuwezaaaa, hawaweziii…,” alisema Lowassa huku akishangiliwa.

Aliongeza kuwa UKAWA ni chombo cha matumaini lakini kina changamoto nyingi za kuhujumiwa na kuwapongeza viongozi kwa kuonesha mshikamano. Alisema UKAWA itafanya kampeni za amani zisizo na fujo wala matusi na kushinda uchaguzi.

“…Kama ni amani kuvurugika haitatokea kwetu itatokea kwao…Nimekuja kujiunga nanyi nikiwa na sababu, sababu hiyo ni ya kuiondoa CCM madarakani laniki tutaweza kuwaondoa kama tunaumoja na mshikamano tukiamini tunaweza,” alisema.

Kwa upande wake mgombea mwenza, Haji alisema UKAWA ndiyo ufumbuzi wa kweli wa kuiangusha CCM na ndio maana wameamua kushirikiana kwa pamoja. Alisema mwaka 1961 wakati nchi ikipata uhuru hakukuwa na makundi kama wamachinga, changudoa, majambazi wala panya road lakini hayo yote yameibuka baada ya watoto masikini kushindwa kujua la kufanya huku Serikali iliyopo madarakani ikiangalia umasikini huo. “…Hayo yote ni matokeo ya utawala wa CCM,” alisema Haji.

Alisema inachofanya CCM ni kuhakikisha Watanzania wanabaki masikini ili waendelee kuwatawala hivyo kuwataka wananchi kuunga mkono ushirikiano wa UKAWA ili kuleta ukombozi wa kweli kwa taifa. Alisema yupo tayari kushirikiana na Lowassa kuzunguka nchi nzima kuwaeleza wananchi waiamini CHADEMA kupitia UKAWA na hatimaye ichukue dola.