UKAWA Wamkaribisha Edward Lowassa Kujiunga, Wapo Tayari Kushirikiana

Baadhi ya viongozi wa UKAWA wakizungumza na vyombo vya habari Makao Makuu ya Chama cha Wananchi, CUF jijini Dar es Salaam leo.

Baadhi ya viongozi wa UKAWA wakizungumza na vyombo vya habari Makao Makuu ya Chama cha Wananchi, CUF jijini Dar es Salaam leo.

Wenyeviti wa CUF, Prof. Lipumba (kulia) na Mbowe wakizungumza jambo kwenye mkutano wa UKAWA na vyombo vya habari leo.

Wenyeviti wa CUF, Prof. Lipumba (kulia) na Mbowe wakizungumza jambo kwenye mkutano wa UKAWA na vyombo vya habari leo.

Na Joachim Mushi, Dar es Salaam

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) unaoundwa na vyama vya CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD umemwalika rasmi Mbunge wa Monduli CCM na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa kujiunga na umoja huo ili waweze kuongeza nguvu ya kuing’oa CCM katika Uchaguzi Mkuu utaofanyika Oktoba 2015.

Ukawa wametoa mwaliko huo leo jijini Dar es Salaam walipokuwa wakizungumza na vyombo vya habari na kudai kiongozi huyo alionewa, kudhalilishwa, kukandamizwa katika uchujo wa CCM kupata mgombea wa urais atakaye peperusha bendera ya chama hicho.

Akitoa tamko la UKAWA, kwa niaba ya wenyeviti wa UKAWA, Mwenyekiti wa Taifa NCCR-Mageuzi, James Mbatia (Mb) alisema njia pekee ya kuing’oa CCM madarakani kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015.

“…Tunachukua fursa hii ya kipekee kumwalika Waziri Mkuu mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mheshimiwa Edward Lowassa ajiunge na UKAWA na tuko tayari kushirikiana naye katika kuhakikisha tunaiondoa CCM madarakani katika uchaguzi mkuu ujao. Tunaamini mheshimiwa Lowassa ana uwezo wa kuhamasisha umma kuikataa CCM yenye kusimamia mifumo isiyotenda haki. Ni mchapakazi makini na mfuatiloaji wa karibu wa utendaji katika majukumu anayokabidhiwa.” Alisema Mbatia katika taarifa ya UKAWA.

“Ni lengo la UKAWA kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu na tutaweka mgombea mmoja wa udiwani katika kila kata na wadi, mgombea mmoja wa uwakilishi na ubunge katika kila jimbo, na mgombea mmoja wa Urais Zanzibar na mgombea mmoja wa Urais wa Jamhuri ya Muungano UKAWA ndilo Tumaini la Watanzania,” alisema Mbatia akiwa na viongozi wakuu vya vyama hivyo vyote.

Aidha aliongeza kuwa Watanzania wanaitaji mabadiliko yatakayojenga demokrasia ya kweli na kuachana na uonevu, udhalilishaji, fitna na majungu yanayoendelezwa na CCM. Alisema uchaguzi wa Oktoba 2015, ukitumiwa vizuri na kimkakati utaleta mabadiliko makubwa yanayotakiwa na wananchi, uchaguzi huu ni fursa muhimu ya kujenga mshikamano wa kitaifa.

UKAWA inaamini katika kuweka mbele maslahi mapana ya wananchi kwa kujenga mshikamano ndani na nje ya vyama vyetu tunapoelekea katika uchaguzi mkuu na hata baada ya Uchaguzi Mkuu.

“Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 ni fursa ya kipekee ya kuleta mabadiliko makubwa katika nchi yetu ya kuondoa mfumo kandamizi uliojikita ndani ya CCM Watanzania wanahitaji mabadiliko yatakayo wapatia Serikali madhubuti yenye fikra mpya na bunifu kwa maslahi yao,” alisema.

Picha zinazodaiwa Lowassa kuonekana kwenye mkutano wa CHADEMA jana usiku, hata hivyo viongozi wa CHADEMA wamezipinga picha hizo na kudai zimetengenezwa.

Viongozi hao wa UKAWA walipoulizwa na wanahabari kwamba mbona Lowassa wanayemwalika anatuhuma mbalimbali za ufisadi walidai ni mfumo ndio uliomchafu hivyo kama kuna mtu mwenye ushahidi kuwa kiongozi huyo anatuhumiwa apeleke vithibitisho.

Hata hivyo taarifa katika mitandao ya jamii zimezagaa zikidai tayari kiongozi huyo (Lowassa) ambaye alionekana kuwa na mvuto mkubwa kwa wananchi katika ziara za kusaka wadhamini ndani ya CCM tayari amefanya mazungumzo na Chadema kwa ajili ya kujiunga na chama hicho jana usiku.

Zipo picha zinaonesha Lowassa akiwa katika kikao cha Chadema jana usiku kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Pamoja na hayo Chadema wamekana taarifa na picha hizo kwamba ni za kizushi na wamedai hata picha inayosambaa ya Lowassa katika mkutano wa Chadema imetengenezwa.