VYAMA vitatu vikuu vya upinzani vinavyounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) vimefanya mkutano mkubwa jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Jangwani huku vikianisha mapungufu yalio katika Katiba Inavyopendekezwa iliyopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba hivi karibuni mjini Dodoma.
Vyama hivyo vya CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi pamoja na chama cha NLD viliongozwa na viongozi wao wakuu pamoja na idadi kubwa ya wananchi kutoka maoneo anuai ya jiji la Dar es Salaam wakiwa ni wafuasi wa vyama hivyo. Vyama hivyo kwa pamoja vilisaini hati ya makubaliano ya kushirikiana ili kuweza kukitoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM). Wakizungumza katika hotuba zao viongozi hao waliwashawishi wananchi kuipinga katiba hiyo utakapofika wakati wa kuipigia kura za maoni kwa madai haijakidhi matakwa ya wananchi.
Walisema rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni kutoka kwa Tume ya Kukusanya Maoni ya Wananchi ilikuwa ina maoni ya wananchi lakini baada ya kujadiliwa na Bunge la Katiba limechakachua na kuweka matakwa yao tofauti na walivyopendekeza wananchi.
Akizungumza mmoja wa viongozi toka CHADEMA, Tundu Lisu aliwataka wananchi kuipiga katiba iliyopendekezwa kwa kuwa kwa sasa haina maoni ya wananchi zaidi ya maoni ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
“…Wakati Rasimu ile inawasilishwa Katiba Bunge Maalum la Katiba ilikuwa na mapendekezo ya Wananchi kweli lakini baada ya kuipitia wajume wale wameibadili kabisa…mule hakuna naoni yenu tena zaidi ya maoni ya Chama Cha Mapinduzi…wanadai ndani ya ile katiba kuna haki za wazee, haki za wanawake haki za kupata elimu na haki za vijana ni uwongo mtupu, huwezi kusema kuna haki wakati hakuna sehemu ya kuzidai haki hizo zinaposhindwa kutekelezwa.
Kwa upande wake Ismail Jussa kutoka CUF aliiita katiba iliyopendekezwa kuwa ni Katiba ya Mzee wa Vijiseti (akimaanisha Katiba ya Andrew Chenge aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Katiba iliyopendekezwa), alidai katiba hiyo haina tofauti na katiba ya mafisadi hivyo kuwataka wananchi waipinge vikali kwenye kura za maoni wakati utakapowadia.
Mkutano huo mkubwa wa vyama hivyo ambao ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa vyama vyote vitatu, yaani Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, Freeman Mbowe wa CHADEMA na James Mbatia wa NCCR-Mageuzi ulilenga kuipinga katiba iliyopendekezwa kwa madai umepuuza maoni ya wananchi.