Ukatili kwa Mwanafunzi; Waziri Amuadhibu Mkuu Sekondari ya Kutwa Mbeya

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, George Simbachawene akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa maagizo kwa Wakurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuwa waanze zoezi la kubainisha mipaka ya asili ya maeneo yote na kuyapima na kuhakikisha yana hati. Picha na Eliphace Marwa - Maelezo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, George Simbachawene akisisitiza jambo.

Na Frank Shija, MAELEZO.

MAMLAKA husika ya nidhamu kwa walimu imeagizwa kumvua madaraka Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kutwa ya Sekondari ya Mbeya, Mwl. Magreth Haule kufuatia kutotoa taarifa juu ya tukio la kushambuliwa kwa mwanafunzi Kidato cha tatu Shule hiyo Sebastian Chingulu.

Ikizungumza na mwandishi maalum kutoka Idara ya Habari –MAELEZO, Jijini Dar es Salaam ambapo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. George Simbachawene amesema kuwa tukio hilo ni la kweli lilitokea tarehe 28 Septemba, 2016 lakini Mwalimu Mkuu huyo akutoa taarifa, hadi ziliposambaa kwenye mitandao ya kijamii.

“Ninaagiza mamlaka husika za kinidhamu kumvua madaraka mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mbeya Kutwa Mwl. Magreth Haule avuliwe madaraka kutokana na kukaa kimya huku kukiwa na tukio la unyama dhidi ya mwanafunzi”. Alisema Simbachawene.

Alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa za awali zilizopatikana tukio hilo lilitokea huku ikidaiwa chanzo chake ni mwanafunzi Sebastian Chingulu kugomea adhabu aliyopewa na mwalimu wake. Aliongeza kuwa walimu waliohusika na tukio hilo ni wa mazoezi kutoka Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambapo walishirikiana kumshambulia mwanafunzi huyo.

SImbachawene aliwataja walimu hao wa mazoezi kuwa ni pamoja na Frank Msigwa kutoka DUCE, ambaye ndiye chanzo kikubwa kufuatia madai ya mwanafunzi huyo kugoma kufanya adhabu aliyopewa na mwalimu huyo. Wengine ni John Deo na Sante Gwamoka kutoka DUCE,mwingine ni Evans Sanga kutoka Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Awali akielezea hatua ambazo tayari Serikali imekwisha zichukuwa, alisema kuwa ni pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya kuendelea na ufuatiliaji wa karibu suala hilo ambapo mpaka sasa vyombo vya dola vinaendelea kuwahoji baadhi ya walimu washule hiyo.

Hatua nyingine ni pamoja na kuendelea kuwasaka wahusika wa tukio hilo kwa kuwa mara baada ya kufanya shambulio hilo walitoweka kusikojulikana, hata hivyo halisisitiza kuwa hakuna hatakaye kwepa katika hili.
Katika hatua nyingine Simbachawene aamewaagiza Wakuu wa Shule za Serikali nchini kuzingatia kanuni za utoaji wa adhabu kwa wanafunzi badala ya kufanya kazi kwa mazoea.