NDIVYO. Hii haina mjadala kabisa. Kama ukisikia moto huharibu vyakula katika mapishi basi kinyume chake ni kuwa ukila vyakula visivyopikwa utakuwa umegeuza mambo na utakuwa umeupa mwili wako vitu adimu sana kwa maisha yetu ya leo ambayo bila moto watu hawakai mezani.
Unapozungumzia urembo basi ujue unagusa mambo matatu: yaani utulivu wa akili, mwili na roho pia. Unapokula vyakula visivyopikwa hakika unautendea mwili wako vema kwani haitakuchukua muda mrefu kabla hujabadilika akili, ngozi, macho, afya kwa ujumla na hata furaha huongezeka pia. Mrembo yeyote ni lazima atimie idara hizo zote yaani kila siku atatakiwa ale angalau 80% ya mlo wake ukiwa ni vyakula visivyopikwa.
Naandika makala hii kwa mapenzi makubwa yenye nia ya kuwaamsha wanawake wote wenye hamasa ya urembo kuwa katika hali ya kawaida ukitaja ‘urembo’ watu hukimbilia kuongea juu ya vipodozi na kuacha urembo halisi na asilia ukijificha ndani ya vyakula vibichi nikimaanisha vyakula ambavyo huwa havipikwi na hasa kachumbari ambayo leo tutaizungumzia kwa undani zaidi.
Kachumbari ni silaha kali sana ya kulinda urembo wako – yaani ngozi, macho, kucha, mwili wenye afya, furaha na vyote ambavyo mrembo anatakiwa awe navyo. Urembo huu hupatikana kirahisi sana endapo utakuwa muumini wa kula kachumbari kila siku yenye nyanya, kitunguu, karoti, ndimu, pilipili na rosemary pia ukipenda. Hivi ni vyakula rahisi, bei nafuu, vinapatikana kirahisi, na haikuchukui zaidi ya dakika tano kuandaa mlo huu na ukafurahisha mwili wako kwa virutubisho sahihi bila gharama kama ilivyo kwa vipodozi.
Kwa leo ningependa kudadavua vilivyomo katika vyakula hivyo na ni kwa jinsi gani vinafanya maajabu ya kuponya, kulinda na kuuremba mwili wa binadamu ila sitaweza kuvitaja vyote nisije kukuchosha. Nitaongelea kitunguu na Mungu akituweka hai basi juma lijalo tuta dadavua kingine na taratibu kwa mfululizo wa makala hizi utapata faida za kiafya zote zilizomo katika vyakula vinavyotengeneza kachumbari.
Kitunguu si kigeni machoni pa wengi. Kitunguu kinapatikana sokoni, gengeni na hata katika baadhi ya maduka na Supermarkets zinazochipuka hivi sasa. Kitunguu ni moja ya vyakula vinavyoliwa duniani toka kabla binadamu hajajua namna ya kuhifadhi kumbukumbu! Hii inamaanisha binadamu alijikuta akianza kutunza rekodi za dunia huku akijikuta ameshakula kitunguu kwa miaka isiyoeleweka idadi. Kitunguu hutumika kama kiungo kwa wengi ili kuongeza ladha ya vyakula vingine na hata kukamilisha mlo uitwao kachumbari utahitaji kitunguu kwanza. Kitunguu ni chakula, ila ni dawa kali ambayo wataalamu wa afya duniani wanakiri kuwa kina nguvu zaidi ya sindano ya penicillin katika tiba za vyakula na hasa katika suala zima la urembo na ulimbende.
Kitunguu kwa ujumla wake kikikatwa, kinatoa harufu kali sana toka mzizi, shina na hata majani yake. Kitunguu hasa ni sehemu yam mea inayofukiwa na udongo shambani na hapo chini huvimba kwa kuongezeka ukubwa wake kadiri kinavyozidi kukua na kwa kawaida kitunguu hulimwa mara moja tu kwa mwaka.
Tunapoongelea urembo sasa, tunatakiwa tuangalie mambo mengi sana ambayo yanatakiwa yafanyike ili mtu apendeze na avutie ikiwemo mavazi, vidani, viatu, vipodozi n.k. lakini huwezi kutaja urembo katika ngozi isiyovutia na yenye maradhi pia. Kitunguu kikiliwa kila siku basi haitakuchukua muda mrefu kuona maradhi ya ngozi yanaisha na badala yake utajikuta uking’aa na kupendeza bila kutumia kipodozi cha aina yoyote. Lakini, ngozi yako itawachanganya sana watu kwa kuwa kitunguu kitakupa mng’aro wa ngozi wa asili kabisa na sio wa kununua dukani.
Nirahisi sana kuthibitisha hili. Kwa kuwa ukila kitunguu kitarahisisha mzunguko wa damu mwilini kwa kusafisha njia zote, basi ngozi haitapendeza kwa kung’ara tu, bali utapendeza kwa kuwa kitunguu kitaua hata minyoo wote ambao kwa kitaalamu huharibu sana ngozi, akili, na kumfanya mtu aonekane amezubaa na kujikunakuna kila mahali, kila mara na kwa haraka wengine hujikuta na mapunye kabisa ambayo ni aina ya minyoo iitwayo ‘ring worms’ na hapo urembo wa mwanamke hupotea.
Ili ufanye jaribio la haraka kujua nguvu ya kitunguu, kikate katikati na kiminye ujipake majimaji yake mwili mzima kwa siku tano hadi saba na hakika utaona maajabu yake kwani utapata fursa ya kuijua ngozi yako halisi. Lakini, usitegemee maajabu ya kulala na kuamka mrembo, maajabu ya kitunguu yatachelea kidogo kulingana na idadi ya seli za ngozi zilizokufa endapo utakuwa nazo nyingi basi matokeo yanaweza kuchelewa hata majuma mawili.
Ukitaja urembo pia unataja masikio mazima. Mrembo kama hasikii vizuri ni tatizo. Huyu anaweza akakamulia juisi ya kitunguu kwenye sikio kila baada ya kuoga na atapata matokeo mazuri ndani ya wiki au mbili hivi hata kama sikio lilikuwa linavuja usaha kabisa litapona. Ni maradhi mengi sana ambayo yanaweza kutibika kama utakula kitunguu kimoja tu kila siku na hasa matatizo ya ngozi pamoja na ulinzi wa ngozi pia.
Maajabu ya kitunguu hutokana na utajiri wa virutubisho na madini pamoja na vitamin zake. Kitunguu kwa mara ya kwanza kilibatizwa jina na Wataliano wakakiita “Onio” na Wafaransa wakakiita “Oignon” wakimaanisha ni chakula pekee chenye maajabu ya tiba na kinga pia.
Pamoja na utajiri wa madini na vitamin zake, kitunguu kina protini kidogo sana ila kina kalsiam na riboflavin kwa wingi mno. Hii hutegemea na kitunguu kukomaa sawasawa, kutokaa ghalani kwa muda mrefu na hata aina ya kilimo kilichozalisha ukichukulia wakulima wengi wa kisasa wapo kibiashara zaidi. Harufu kali ya kitunguu hutokana na kiasi kikubwa cha madini ya asili ya salfa yaliyosheheni na haraka tu utagundua kuwa salfa ni dawa ya binadamu, mimea, hasa kukinga wadudu wanaoshambulia majani na matunda pia hivyo kitunguu kikitumika kwa urembo basi ujue utasahau bei za lotion na mikorogo kwa ujumla utakuwa mrembo wa kufa mtu!
Ila bado kitunguu kina tindikali ziitwazo ‘amino’ ambazo dunia ya wataalamu wa afya wameshindwa kutengeneza fomula yake na kubaki ni siri kati ya binadamu na Mungu tu kwa kuwa Amino humfanya mtu kuwa na furaha, tabasamu na mchangamfu muda wote. Warembo mpo hapo?
Hatutatenda haki endapo tutazungumza urembo bila kugusa meno. Meno ndio yanamfanya mtu yeyote kuvutia. Ukiwa na mapengo hupendezi. Kama utakuwa muumini wa kachumbari basi amini kuwa utakuwa ukiwafukuza wadudu waharibifu wa meno wote mdomoni na hutapata maradhi ya meno wala fizi kamwe.
Hii itahusisha kutafuna kitunguu hicho kwa kukizungusha mdomo wote ili dawa iingie kila mahali. Pamoja na kujikinga na maradhi ya meno, kama ulikuwa ukitoa harufu mbaya mdomoni basi ujue ugonjwa huo utapona haraka sana kwani hata jino likiuma ni rahisi kulitibu kwa kutafunia kitunguu tu eneo hilo kila baada ya masaa mawili na siku hiyohiyo utaanza kujisia nafuu nap engine ukapona kabisa. Ila ni vema tungeona kitaalamu kitunguu kina vitu gani mpaka kitoe maajabu haya?
Kitunguu
Faida zake Madini & Vitamins
Moisture 86.6% Calcium 47 mg
Protein 1.2% Phosphorus 50 mg
Fat 0.1% Iron 0.7 mg
Fibre 0.6% Vitamin C 11 mg
Minerals 0.4% Vitamin B Complex Small ammount
Carbohydrates 11.1% Calorific Value 51
*value in 100gram 100%
Nafikiri nisikuchoshe sana msomaji wangu. Ila nikuahidi tu kuwa juma lijalo tukutane tena hapa ili tuweze kudadavua faida zilizomo katika vyakula vingine vinavyotumika kutengeneza kachumbari ambapo tutaongelea kila aina ya chakula kwa wiki na hivyo tutamaliza makala hii baada ya wiki tano au sita. Nakusihi sana usikae mbali nasi.
Alamsiki…
Imeandaliwa na John Haule