TIMU ya Taifa ya Ujerumani imefanya mauaji ya kihistoria katika Fainali za Kombe la Dunia baada ya kuibugiza Timu ya Brazil mabao saba kwa moja (7-1). Katika mchezo huo wa Nusu Fainali Ujerumani wakionesha kasi kubwa ya mchezo wa kushambulia kwa makini ndani ya dakika 29 za kipindi cha kwanza tayari walikuwa na magoli na magoli matano.
Magoli ya Ujerumani yalikuwa yakifungwa mfululizo kuanzia dakika ya 11 ya mchezo kipindi cha kwanza ambapo mchezaji nyota na muhimu wa Ujeruman Muller alifungua kitabu cha magoli katika dakika ya 11 ya mchezo. Timu ya Brazil ambayo ilicheza kwa kukata tamaa baada ya kuruhusu magoli ya matano ndani ya dakika 29 za kipindi cha kwanza, ilijikuta ikipoteza muelekeo jambo ambalo lilizidi kuwapa nguvu wapinzani wao.
Brazil ikicheza bila mshambuliaji wao nyota, Neymar ilijikuta ikimaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza ikiwa tayari imeshindiliwa magoli 5 kwa bila. Wauaji wa Brazil walikuwa ni pamoja na Muller dakika ya 11′, Klose dakika ya 23′, Kroos dakika ya 24′ na 26′ na pia Khedira katika dakika ya 29′.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu ya Brazil kujitahidi kuondoa aibu hiyo kwa kushambulia kwa kasi bila umakini na kujikuta washambuliaji wake wakishindwa kufunga katika nafasi walizozipata. Ujerumani iliendeleza mauaji tena kipindi cha pili ambapo Schurrle akitokea bechi aliingia na kufunga magoli mawili tena katika dakika za 69′ na 79′.
Mashabiki wa Brazil walionekana kuanza kuondoka mapema kuanzia mwisho wa kipindi cha kwanza baada ya ubao wa matokeo kosoma 5-0. Kocha Mkuu wa Brazil, Felipe Scolari alionekana kukata tamaa dakika ya 70 baada kuona wachezaji wake wakipoteza muelekeo huku idadi ya magoli yakiongezeka. Mchezaji wa Brazil, Oscar katika dakika ya 90′ aliifuta machozi timu yake kwa kujipatia bao la kwanza, goli ambalo lilishangiliwa na mashabiki wake.
Hadi mwisho wa mchezo huo uliopigwa katika dimba la Estadio Mineirao, mjini Belo Horizonte, nchini Brazil, timu ya Ujerumani ilijipatia magoli 7 huku Brazil ikiambulia goli moja.