Ujenzi wa shule za kata waleta vituko elimu ya sekondari

Baadhi ya wanafunzi wa shule za kata wakiwa mapumziko shuleni

Na Joachim Mushi
Rukwa

UJENZI wa Shule za Sekondari kwa kila Kata maarufu kama ‘sekondari za kata’ katika mikoa anuai umeongeza vituko kwenye sekta ya elimu kwa baadhi ya maeneo kwani kutokana na upungufu mkubwa wa walimu hasa wa masomo ya sayansi na lugha baadhi ya shule zimefuta masomo hayo kinyume na taratibu za mitaala.

Miongoni mwa mikoa iliyokubwa na kadhia hiyo ni Rukwa, Wilaya ya Nkansi ambako baadhi ya shule hizo zimekata tamaa baada ya kukosa walimu wa sayansi na kulazimika kufuta masomo ya sayansi na kubaki na yale ya sanaa, licha ya kwamba nayo si yote yenye walimu kwenye shule hizo.

Uchunguzi uliofanywa mwandishi wa habari hizi, hivi karibuni wilayani Nkasi na baadaye kuthibitishwa na Ofisa Elimu Sekondali wilaya hiyo, Abel Ntupwa umebaini hilo.

Uchunguzi umebaini idadi kubwa ya shule za sekondari za kata hazina walimu wa masomo ya sayansi yakiwemo Fizikia, Kemia, Hesabu pamoja na somo la Kiingereza hali inayosababisha baadhi ya shule kutafuta wanafunzi wa kidato cha nne na tano kusaidia kufundisha masomo hayo kwenye shule ambazo bado zinajitutumua kufundisha masomo hayo.

Katika baadhi ya shule ambazo zilitembelewa na gazeti hili ikiwemo Shule ya Sekondari ya Mkole iliyopo nje kidogo ya Mji wa Namanyele wilayani Nkasi, mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne ndiye anayefundisha somo la Hisabati takribani vidato vyote vya shule hiyo, huku somo la Kiingereza likiwa halina mwalimu kabisa.

Shule nyingine ambazo masomo ya sayansi yanafundishwa na wanafunzi wa kidato cha nne ni pamoja na Mashete Sekondari, ambayo Frank Kapangala aliyemaliza kidato cha nne mwaka 2010 anafundisha Hisabati na Baiolojia kidato cha kwanza na cha pili. Akizungumza na Jambo Leo shuleni hapo Kaimu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Raban Kapandila alisema licha ya juhudi binafsi za walimu kumchukua mwanafunzi huyo wa kidato cha nne kufundisha hali bado ni mbaya zaidi shuleni hapo.

Kapandila alisema masomo kama Fizikia na Kemia hayana walimu kabisa na hayafundishwi katika shule hiyo yenye kidato cha kwanza na cha pili na jumla ya wanafunzi 90, huku akibainisha huenda masomo ya Hisabati na Baiolojia yakaachwa kufundishwa tena kwani Kapangala anatarajiwa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu kuendelea na masomo yake.

Akizungumza na mwandishi ofisini kwake, Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Nkasi, Abel Ntupwa alikiri kuwepo na upungufu mkubwa wa walimu hasa masomo ya sayansi na lugha hali inayochangia baadhi ya shule kukosa walimu wa masomo hayo. Ntupwa alisema kutokana na hali hiyo zipo baadhi ya shule wilayani hapo zimekata tamaa ya kupata walimu wa sayansi na kuamua kuondoa masomo hayo na kubaki na mchepuo wa masomo ya sanaa.

“Ni kweli zipo baadhi ya shule zimeondoa masomo ya sayansi na kubaki na masomo ya sanaa kutokana na kukosa walimu wa sayansi kwa kipindi kirefu…zipo shule zimefikia hatua hiyo naweza nikakutajia,” alisema Ntupwa.

Akitoa ufafanuzi a liongeza kuwa juhudi zimekuwa zikifanywa katika ngazi mbalimbali za wilaya hiyo na ndio maana baadhi ya wanafunzi wenye uwezo wamekuwa wakiingia makubaliano na uongozi wa shule na kusaidia kufundisha na pengine walimu waliosomea masomo mengine kupewa masomo ya sayansi kwa makubaliano endapo walikuwa na historia nzuri za masomo hayo kidato cha nne au cha tano.