Ujenzi Makao Makuu Mahakama ya Afrika Kuharakishwa

Jaji Augostino Ramadhani

Jaji Augostino Ramadhani


 
Na Mtua Salira, EANA – Arusha

RAIS wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) Jaji Augostino Ramadhani alikutana mwishoni mwa wiki na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine walijadili namna ya kuongeza kasi ya ujenzi wa makao makuu ya mahakama hiyo.
 
Tanzania kama mwenyeji wa mahakama hiyo, itajenga makao katika eneo la Kisongo, nje kidogo ya jiji la Arusha. Imeelezwa kwamba serikali tayari imekamilisha michoro ya ujenzi wa mahakama hiyo. Hivi sasa mahakama hiyo inafanyakazi kutoka makao yake ya muda yaliyopo ndani ya ofisi za makao makuu ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), eneo la Burka jijini Arusha tangu 2007.
 
Rais Kikwete pia alipewa taarifa fupi za shughuli za mahakama hiyo na kujadili namna ya kuboresha uelewa wa raia juu ya uwepo wa mahakama hiyo barani Afrika, Shirika Huri la Habari la Afrika Mashariki (EANA) limenukuu taarifa iliyotolewa na mahakama hiyo kwa vyombo vya habari.
 
Tangu makubaliano ya kanzishwa kwa mahakama hiyo zaidi ya miaka 17 iliyopita, ni nchi 28 tu kati 54 wananchama wa Umoja wa Afrika (AU) ndiyo zilizoridhia mkataba wa kuanzishwa mahakama hiyo ambapo pia nchi saba zimeruhusu watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali(NGOs) kufungua kesi katika mahakama hiyo.
 
Mafanikio ya mahakama hiyo kama chombo cha kupigania haki za binadamu unahitajika uungwaji mkono na nchi wananchama kwa kuridhia uwepo wake. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Umoja wa Wanasheria Afrika, Don Deya anasema kuridhiwa kwa mkataba huo na nchi zote wanachama wa AU kutaiwezesha mahakama hiyo kutekeleza majumu yake kwa ufanisi.