Uingereza Yamwalika Rais Kikwete Kuwatembelea
UINGEREZA imemwalika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa ziara rasmi kutembelea nchi hiyo kwenye sehemu ya kwanza ya mwaka huu, 2014. Rais Kikwete amekubali mwaliko huo.
“Tunakualika rasmi na kukuomba Mheshimiwa Rais uwe mgeni wa Serikali ya Uingereza wakati wowote katika sehemu ya kwanza ya mwaka huu,” Waziri wa Mambo ya Nje na Jumuia ya Madola wa Uingereza, Mheshimiwa William Hague amemwambia Rais Kikwete ambaye naye ameukubali mwaliko huo.
Waziri Hague ametangaza hatua hiyo ya Uingereza kumwalika leo, Jumatano, Februari 12, 2014, Rais Kikwete wakati Rais Kikwete alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri huyo kwenye makao makuu ya wizara hiyo mjini London, Uingereza.
Mkutano huo kati ya Rais Kikwete na Waziri Hague ndio umekuwa shughuli ya kwanza ya Mheshimiwa Rais Kikwete kwenye ziara yake ya siku tatu nchini Uingereza baada ya kuwa amewasili nchini Uingereza asubuhi ya leo.
Shughuli kubwa ya Rais Kikwete katika ziara hiyo itakuwa ni kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Kujadili Jinsi ya Kukomesha Ujangili na Mauaji ya Tembo na Faru Duniani unaofanyika kesho, Alhamisi, Februari 13, 2014, katika Jumba Maarufu la Kihistoria la Lancaster House mjini London.
Wakati wa mazungumzo hayo, Waziri Hague pia amempongeza Rais Kikwete kwa msimamo wake na uongozi wake katika mapambano dhidi mauaji ya tembo na faru duniani akisema kuwa uongozi huo sasa umeanza kuzaa matunda.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete amemwelezea hatua ambazo zimekuwa zinachukuliwa na Tanzania tokea miaka ya 1988 kukabiliana na tatizo la ujangili ambalo limepunguza idadi ya tembo wa Tanzania kutoka 350,000 katika miaka ya 1960 kufikia chini ya 100,000 kwa sasa.
Rais Kikwete pia amemwambia Waziri Hague kuwa Tanzania sasa imeachana na msimamo wake wa miaka ya nyuma kidogo ya kujaribu kuuza tani 180 za meno ya tembo ambao walikufa wenyewe miaka ya nyuma. “Msimamo wa sasa ni kwamba hatutajaribu tena kuuza meno hayo.”
Viongozi hao wawili pia wamejadili mambo mengine likiwamo suala la majadiliano ya kufikia Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) kati ya Jumuia ya Ulaya (EU) na Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na masuala mengine yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Uingereza.