Uingereza yaionya Algeria

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague

WAZIRI wa mambo ya nje wa Uingereza , William Hague, ameitaka Algeria iheshimu sheria ya kimataifa kwa kuwakabidhi watoro wa vita nchini Libya.
Mke wa Kanali Gaddafi na wanawe watatu walivuka mpaka wa Algeria wakikimbia mapambano nchini Libya mnamo mwezi wa Agosti.
Akiongea baada ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Bwana Hague aliwaonya viongozi wa Algeria kutowapa hifadhi watoro kutoka Libya ambao wanatafutwa na Mahakama ya Jinai ya kimataifa.
Bwana Hague aliwasili Algeria mnamo siku ya Jumanne katika ziara ya nchi za Kaskazini mwa Afrika ambapo amekwishazizuru Libya, Morocco na Mauritania.
Algeria inapaswa kushirikiana na watawala wa Libya kwa ombi lolote watakalolitoa, alisema na kuongeza kwamba nchi yoyote katika kanda hiyo ambayo itawapa hifadhi watoro wa mahakama ya kimataifa wanapaswa kuwakabidhi.
Mkewe Kanali Gaddafi, Safia, binti yake Aisha na wanawe wawili wa kiume, Hannibal na Mohamed,walikimbia wakiwa na takriban jamaa zao 20 na kuingia Algeria mnamo mwezi wa Agosti.
Wanadhaniwa wako katika mji wa jangwani wa Illizi.
Serikali ya Algeria inasema imewachukua kwa sababu za kibinaadamu lakini hatua hiyo imezusha uhasama kati ya Algeria na viongozi wapya wa Libya.
Inadhaniwa kwamba viongozi wa Libya wataomba jamaa wa familia ya Gaddafi wakabidhiwe kwao katika wiki chache zijazo.
Kwa upande wake Algeria imesema haitampa hifadhi Kanali Gaddafi ama yeyote anaetafutwa na mahakama ya Kimataifa.

-BBC