UINGEREZA imeahidi kuzijengea uwezo nchi zinazoendelea ili ziweze kutambua thamani ya maliasili zake kwa kuwataka wawekezaji katika nchi hizo kulipa kodi inayostahili, kuweka uwazi katika mapato yanayotokana na maliasili hizo na kuweza kuthaminisha ardhi ya nchi hizo kwa manufaa zaidi.
Aidha, Uingereza inataka nchi zinazoendelea kutokuwauzia wawekezaji ardhi bali ziwe na uwezo wa kutumia ardhi yake na kuithaminisha kama kitega uchumi chake kwa manufaaa zaidi.
Msimamo huo wa Uingereza ulielezwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron katika mkutano wa viongozi wachache wa Afrika ambao wamekuwa wanakutana na Waziri Mkuu huyu kumweleza matakwa ya Afrika ambayo yatawasilishwa katika Mkutano wa Viongozi Nchi Tajiri na Zenye Viwanda Vingi Zaidi Duniani (G-8) ulioanza Ireland ya Kaskazini leo, Jumatatu, Juni 17, 2013 na unaofanyika kwa siku mbili.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi hao wachache wa Afrika waliokutana na Waziri Mkuu Cameron ambaye pia ametaka Serikali za nchi zinazoendelea kuonyesha uwajibikaji mkubwa zaidi na uwazi zaidi katika matumizi na mapato ya kodi yanayotokana na maliasili hizo.
Uingereza ndiye mwenyekiti wa G8 mwaka huu na imeliweka suala la biashara, kodi na uwazi katika uwekezaji na biashara kama moja ya agenda yake katika kuzisaidia nchi zinazoendelea. Nchi hiyo ndiyo itawakilisha mawazo na maoni ya Afrika kwenye Mkutano huo wa viongozi wa G-8.
Katika mpango huo, Uingereza inataka kuzishawishi nchi za G8 kusaidia nchi zinazoendelea kujenga uwezo wa kutambua mali asili zilizopo, kutambua thamani yake, kodi inayolipwa na kama inastahili na kuzitaka kampuni zinazowekeza kuwa wazi zaidi katika biashara zao na shughuli wanazofanya ili nchi na watu wake ziweze kufaidika na mali asili yake.
Nchi wanachama wa G8 ni Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan,Urusi, Marekani na Uingereza
Mbali na mkutano huo wa baadhi ya nchi za Afrika na Bw. Cameron, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Sir. Richard Branson, mfanyabiashara mkubwa na bilionea wa uingereza ambaye ni mwenyekiti wa Kundi la Makampuni ya Virgin yanayoendesha shughuli mbali mbali ukiwamo usafiri wa anga na reli.
Rais amefanya mazungumzo na Bw. Branson kwa nia ya kumshawishi kuwekeza Tanzania katika masuala ya anga, kupitia kampuni yake ya Virgin Atlantic Airways ambapo Bw. Branson ameahidi kufanyia utafiti suala hilo lakini pia ameonyesha nia ya kuwekeza kwenye reli.
Rais Kikwete pia ametembelea makao makuu na uwanja wa timu ya soka la Sunderland na kujionea jinsi vijana wadogo wanavyopata mafunzo na kuendeleza vipaji vyao vya mpira.
Kampuni ya umeme ya Symbion imeahidi kujenga shule ya kufundishia na kuendeleza vipaji vya mpira kwa vijana wadogo ambapo timu ya Sunderland imeahidi kutoa mafunzo, walimu na kujenga uwezo kwa watanzania.
Rais amemalizia shughuli zake 17 Juni kwa kukutana na wawekezaji mbalimbali wa sekta ya nishati ambao wamezungumzia masuala mbalimbali ya uwekezaji nchini. Rais Kikwete anatarajia kurejea Dar-es-Salaam Juni 18, 2013.