UHURU WA VYOMBO VYA HABARI HAUTAFIKIWA BILA USAWA WA KIJINSIA

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Bi. Eda Sanga (kushoto) akizungumza alipokuwa akifungua moja ya semina za mafunzo kwa wanahabari juu ya uandishi wa habari za usalama barabarani ofisi kuu ya TAMWA Sinza jijini Dar es Salaam.

 

Na Mwandishi Wetu

KILA ifikapo Mei 3, wanahabari na wadau mbalimbali wa vyombo vya habari duniani huungana kwa pamoja kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.

Wakati tukiadhimisha siku hii muhimu ya wanahabari kuna mambo kadhaa ya kuangalia. Mfano kwa muda mrefu sasa baadhi ya wadau mbalimbali na mashirika anuai wamekuwa wakivitumia vyombo vya habari kama chombo cha ukombozi wa haki za wanawake, watoto na makundi mbalimbali ili waondokane na minyororo ya unyanyasaji na ukandamizwaji wa haki zao za msingi kwa mujibu wa katiba ya nchi na mikataba mbalimbali ya kimataifa kama ilivyosainiwa na kuridhiwa nchini.

Kimsingi katika kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari mwaka huu, naungana na Chama cha Wanahabari Wanawake nchini na mashirika ya kihabari nchini kote pamoja na vyombo vya habari kuvitaka vyombo vya habari kuibua masuala mbalimbali yanayohusu haki za wanawake na watoto.

Ni miaka 30 sasa tangu kuanzishwa kwa TAMWA, ambapo kwa mda wote huo, TAMWA imekuwa ikivitumia vyombo vya habari katika ujenzi wa jamii yenye kuchukua na kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto. Ni ukweli kuwa pamoja na changamoto ambazo bado vyombo vya habari nchini vinapitia, ila nipende tu kuvipongeza kwa hatua iliyofikiwa na vyombo vya habari nchini, kwani kupitia ushawishi na uchechemuzi tumeweza kupata sheria mbalimbali zenye kupinga ukatili kwa kijinsia.

Pamoja mafanikio yaliyotokana na vyombo vya habari kwa upande wa mlengo wa kijinsia, bado tuhitaji kuutumia uhuru wa vyombo vya habari katika mambo makuu mawili. Jambo la kwanza ni kuibua aina mbalimbali za ukatili unaowakumba makundi mbalimbali ndani ya jamii ikiwepo vipigo kwa wanawake, ukeketaji, ulawiti, ubakaji, ndoa za utotoni pamoja na mila kandamizi zilizoota mizizi mirefu tangu siku nyingi.

 

Sehemu ya wahariri na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakiwa katika moja ya mikutano ya mafunzo ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) jijini Dar es Salaam.

Jambo la pili ni pamoja na kuwaibua wanawake na kuwatangaza kuwa wao nao wana zisa stahiki kuwania nafasi mbalimbali za uongozi. Katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ambayo kauli mbiu yake mwaka huu ilikuwa “Fikra Yakinifu kwa wakati Muhimu; Jukumu la Vyombo vya Habari katika kuendeleza Jamii zenye Amani, Haki Jumuishi” TAMWA imewataka wanahabari kote nchini kufanya kazi zao kwa weledi hasa katika kuhakikisha wanazingatia usawa katika kutoa taarifa mbalimbali zikiwemo zile zinazohusu wanawake, watoto na wanaume.

Aidha katika maadhimisho ya mwaka huu, TAMWA inawapongeza wanahabari na vyombo vya habari nchini kwa jinsi vinavyoshirikiana katika kuhakikisha vitendo vya ukatili wa kijinsia vinatolewa taarifa bila woga na wahusika wanachukuliwa hatua stahiki kwakua vitendo hivyo huchangia katika kurudisha nyuma maendeleo ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.

TAMWA katika mpango mkakati wake wa kuelimisha jamii kuondokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto, kwa kipindi cha mwaka 2015 na 2016 wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini zaidi ya 2,350 na wahariri 120 walijengewa uwezo wa jinsi ya kuandika habari za ukatili wa kijinsia zenye kuleta mabadiliko katika jamii ambapo kwa sasa vitendo hivyo vinatolewa taarifa kwa usahihi ukilinganisha na awali.

TAMWA katika kutekeleza mradi wake wa GEWE II kimeweza kuhunda kamati za kuelimisha jamii jinsi ya kushughulikia vitendo vya ukatili wa kijinsia katika wilaya kumi za Tanzania na Bara na visiwani ambazo zinawahusisha wanahabari ili kuziwezesha jamii kushirikiana na vyombo vya habari kuweza kuvitolea taarifa vitendo hivyo bila woga ambapo kamati hizo zimesaidia kuibua matukio hayo.

TAMWA inaamini kuwa kupitia vyombo vya habari na uandishi wenye weledi Tanzania mpya inaweza kujengwa isiyolkuwa na misingi ya unayanyasaji wa kijinsia.