TIMU ya taifa ya Uholanzi imeongeza machungu kwa timu ya taifa ya Brazil katika fainali za kombe la dunia baada ya kuichapa timu hiyo mabao matatu kwa mtungi. Kipigo hicho ambacho ni cha pili mfululizo kwa wa Brazil kimetokea katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu katika fainali hizo.
Timu ya Brazil katika mechi yao ya nusu fainali waliyokutana na timu ya taifa ya Ujerumani walipokea kichapo cha mbwa mwizi baada ya kubugizwa magoli 7-1, kipigo ambacho hakijawahi kutokea katika hatua hiyo kwa timu kubwa kama Brazil.
Washabiki wengi walitegemea Brazil itafuta machungu katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu wa fainali za kombe la dunia kwa kuishinda timu ya Uholanzi jambo ambalo limekuwa kinyume hivyo kujikuta wakipokea kipigo kingine cha mabao 3-0.
Uholanzi walianza kibarua cha kujihesabia magoli mapema katika dakika za kwanza za mchezo huo ambapo iliwachukua dakika 3 tu za mchezo na kutikisa nyavu za Brazil goli ambalo lilifungwa kwa penati na nahodha wa Uholanzi, Robin Van Persie baada ya mchezaji hatari wa Uholanzi, Arjen Robben kuangushwa ndani ya penati boksi.
Mauaji ya goli la pili kwa Uholazi yaliwakumba Wabrazili katika dakika ya 16 ya mchezo ambapo mchezaji Daley Blind alifunga goli hilo lililozidi kuwachanganya wachezaji wa timu ya Brazil na kuanza kuhofia kiama kingine. Hadi timu zote zikienda mapumziko Uholanzi ilikuwa ikiongoza kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili wachezaji wa Brazil waliongeza kasi ya kushambulia katika goli la wapinzani wao na kujikuta wakikosa mabao mara kadhaa, kiwewe kilichowafanya Uholanzi kucheza kwa kujihami zaidi huku wakishambulia kwa kushtukiza. Hata hivyo bahati haikuwa kwa wafungaji wa Brazil hivyo kujikuta wakigeuziwa kibao na kufungwa goli la tatu katika dakika za majeruhi 91 za mchezo huo, lililofungwa na Georginio Wijnaldum.
Hadi mwisho wa mchezo huo Uholanzi 3 na Brazil 0, kwa matokeo hayo timu ya Taifa ya Uholanzi wametangazwa washindi wa tatu wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2014. Hapo baadaye Ujerumani wataingia dimbani kukipiga na Agertina kutafuta mshindi wa kwanza wa fainali hizo.