Na Happiness Shayo – Morogoro
TIMU ya soka ya Uhamiaji imeweka historia katika michezo ya SHIMIWI baada ya kuifunga timu ya soka ya Ikulu bao moja kwa bila katika mchezo wa mtoano uliofanyika viwanja vya Morogoro Sec. mjini Morogoro na hivyo kuitoa timu hiyo ya Ikulu katika mashindano ya SHIMIWI.
Mchezo huo wa aina yake uliochezwa kwa vipindi viwili vya dakika thelathini ulianza kwa kasi huku timu ya Ikulu ikijitahidi kushambulia lango la Uhamiaji kupitia mshambuliaji wake Salehe Hamad bila mafanikio.
Ikulu ambayo inaongoza kwa kunyakua kombe la soka la SHIMIWI kwa mfululizo ilishindwa kufunga bao katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo hivyo hadi timu hizo zinaenda mapumziko hakuna aliyemfunga mwenzake.
Uhamiaji iliyokuwa imeangukia kundi la wafungwa bora kwa kupata pointi 4 katika michezo ya SHIMIWI ilijitoa kimasomaso katika kipindi cha pili cha mchezo huo baada ya mshambuaji wake Edward Dafe kufunga bao la kufuta machozi lililoiingiza timu hiyo katika 16 bora.
Goli hilo la Uhamiaji lilileta changamoto kwa wachezaji wa Ikulu ambao mda wote walipania kunyakua ushindi na kupelekea kucheza rafu hadi kumjeruhi kipa wa Uhamiaji Josia Steven ambaye aliendelea na mchezo baada ya kupewa huduma ya kwanza.
Akiongelea mchezo huo Katibu wa timu ya Uhamiaji, Richard Mwasongwe alisema kuwa mchezo ulikuwa mgumu kwa timu yake lakini jitihada binafsi zimepelekea kuwa na matokeo mazuri.
“Mchezo huu ni mgumu sana lakini timu yangu imejitahidi kadri iwezekanyavyo kufanya vizuri,” alisema.
Kwa upande wa timu ya Ikulu, ilishindwa kutoa ushirikiano wa kuelezea hali halisi ya mchezo huo na badala yake kuondoka uwanjani kwa majonzi.
Timu za soka zilizoingia 16 bora zitaingia dimbani Oktoba 6 ambapo watakaofanikiwa kupita katika hatua hiyo wataingia robo fainali ya mashindano ya SHIMIWI.