HADI sasa Ugiriki haijaweza kupata Serikali na hatima ya nchi hiyo ndani ya sarafu ya euro sasa imo mashakani, baada ya chama cha mrengo wa kushoto kutangaza kushindwa kufikia makubaliano ya kuunda Serikali.
Mpira sasa uko upande wa kiongozi wa chama cha kisoshalisti cha PASOK, Evangelos Venizelos, anayekabiliwa na jukumu lisilo shukurani la kuunda serikali hivi leo, kufuatia kushindwa kwa mpinzani mkubwa wa mpango wa kubana matumizi, Alexis Tspiras, hapo jioni ya jana.
“Hatuwezi kutimiza ndoto yetu ya Serikali ya mrengo wa kushoto. Kesho nitarudisha idhini niliyopewa na rais wa jamhuri ya kuunda serikali na tutaendelea kushiriki katika utaratibu wa kikatiba.” Alisema Tspiras akitangaza kushindwa huko.
Kiongozi wa chama cha mrengo wa kushoto cha Ugiriki, Alexis Tsipras. Mapema vyama vikuu nchini humo vilikuwa vimekataa kushirikiana na Tspiras, ambaye chama chake cha Syriza ni cha pili kwa wingi wa viti bungeni, kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya mpango wa kubana matumizi.
Tspiras aliutangaza mpango wa uokozi wa Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa kuwa haufai, na akaapa angeliuchana mkataba wa makubaliano kati ya nchi yake na Umoja wa Ulaya, hali ambayo imezusha tafrani miongoni mwa viongozi wakuu wa Umoja huo.
“Nchi zilizo kwenye mpango wa uokozi hazina hiyari isipokuwa kudhibiti kufilisika kwa serikali. Na huo ndio msimamo wangu kwamba hakuna njia nyengine zaidi ya kuwa imara kwa kuchukuwa hatua za mageuzi na kuinuwa uwekezaji.” Amesema Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya, Jose Manuel Barosso.
Hata hivyo, kwa wengine ndani ya Umoja wa Ulaya wanaona kwamba sasa uwezakano wa Ugiriki kujitoa kwenye umoja wa sarafu ya euro upo wazi zaidi. Katika mkutano wa Jukwaa la Uchumi la Ulaya, Waziri wa Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle alisema kwamba ni jukumu la Ugiriki yenyewe kuamua nini inataka kufanya kuhusiana na hatima yake kwenye kanda ya euro.
Katika wakati ambao fursa ya kuunda serikali sasa imeangukia mikononi mwa Venizelos, ambaye chama chake cha PASOK kilipata nafasi ya tatu bungeni kwenye uchaguzi wa Jumapili, suali ni ikiwa atawezaje kufanya kile ambacho wenzake wa vyama vilivyopata nafasi za kwanza na pili wameshindwa.
Licha ya waziri huyo wa zamani wa fedha mwenyewe kupigania makubaliano yaliyozaa mpango wa sasa wa kubana matumizi, sasa hata chama chake cha Kisoshalisti kinaonesha dalili za kutaka makubaliano mapya ya masharti ya mpango wa kimataifa wa uokozi.
Wakopeshaji wameionya Ugiriki kwamba deni linalopaswa kulipwa leo litakuwa la mwisho, ikiwa nchi hiyo itarudi nyuma kwenye mageuzi yake machungu ya uchumi. Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Shäuble, amesema “ikiwa Ugiriki inataka kubakia kwenye umoja wa sarafu ya euro, haina njia bora zaidi ya kufanya hivyo kuliko kuendelea kutekeleza makubaliano, akisisitiza kuwa “haiwezi kuchagua kupokea mkopo bila ya kubana matumizi na kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi.”
-DW