Uganda Kuwa Mwenyeweji Mafunzo ya Kijeshi ya EAC

Baadhi ya wanajeshi kutoka nchi za EAC

Na James Gashumba, EANA

UGANDA itakuwa mwenyeji wa mafunzo ya tatu ya kijeshi ya kanda ya Afrika Mashariki mwezi ujao yatakayojumuisha askari 1250 ikiwa ni sehemu ya jeshi litakalokuwa tayari kwa dharura yoyote katika kanda ifikapo 2015, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) limeripoti.

Kikao maalum cha 9 cha Baraza la Mawaziri wa Ulinzi na Usalama wa Kanda ya Mashariki chini ya Kikosi cha Dhurura cha Kanda ya Afrika Mashariki (EASF) kilichoketi Kampala, Uganda mwishoni mwa wiki kimekubaliana kutumia kikosi hicho kufanya mafunzo yake nchini humo. Kikosi hicho kitakuwa chini ya Umoja wa Afrika (AU).

Mafunzo hayo yatafanyika katika kituo cha Ujenzi wa Maendeleo kilichopo Mashariki mwa mji wa Jinja. Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Ulinzi wa Rwanda Jenerali James Kabarebe alitoa wito wa kutafutia suluhisho migogoro iliyopo katika bara la Afrika.

Kikosi cha EASF ni moja ya vikosi vitano vya kanda vya kuwa tayari kukabiliana na majukumu yoyote ya dharura ya AU kwa lengo la kudhibiti migogoro na kuimarisha amani na usalama katika bara la Afrika.

Mkutano huo uliokuwa chini ya uwenyekiti wa Jenerali Kabarebe umekubaliana kutuma kikosi chenye kujumuisha jeshi, polisi na raia kwenye mafunzo hayo ya pamoja ya kijeshi. Mafunzo hayo ya wiki moja yatayojulikana kwa jina la medani la ”Field Training Mashariki Salaam 2013.”

Mamia ya askari wameshachukua mafunzo ya aina hiyo katika awamu ya kwanza na ya pili Sudani Kusini na Djibouti.

“Matukio ya hivi karibuni ya Mashariki mwa DRC, Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati ni mifano hai ya haja ya Afrika kuimarisha uwezo wake wa kujitafutia suluhisho kwa matatizo yake ya migogoro barani Afrika,” alisistiza Jenerali Kabarebe.