Uganda Kuwa Mwenyeji Jukwaa la Katibu Mkuu EAC

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk. Richard Sezibera

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk. Richard Sezibera

Na Mtuwa Salira, EANA-Arusha

UGANDA itakuwa mwenyeji wa mkutano wa tatu wa mwaka wa Jukwaa la Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaoshirikisha sekta binafsi, vyama vya kiraia na wadau mbalimbali, utakaofanyika Mjini Entebe, Septemba 12 hadi 13, 2014.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) uamuzi huo ni miongoni mwa maamuzi yaliyofanywa na Kamati ya Kanda ya Maandalizi ya mkutano huo wenye wajumbe kutoka nchi wanachama wa EAC, Sektretariati ya EAC, sekta binafsi, vyama vya kiraia na wadau kutoka makundi mbalimbali uliofanyika mjini Mwanza mwishoni mwa wiki.

Kamati hiyo pia imechagua kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu kuwa ni “EAC: Nyumbani kwangu, Biashra yangu.” Mkutano wa kwanza wa Jukwaa la Katibu Mkuu wa EAC ulifanyika jijini Dare sealaam, Tanzania, Desemba 2012 na wa pili ulifanyikia Nairobi, Kenya Oktoba, mwaka jana.

Mkutano huo una lengo la kutoa jukwaa la majadiliano baina ya Katibu Mkuu wa EAC na sekta binafsi na wadau wengine wa kanda hiyo juu ya namna ya kuimarisha mtangamanano wa EAC.

“Lengo la jukwaa hili ni kutoa nafasi kwa wadau waliochaguliwa na EAC kushauriana na kufanyia kazi masuala yanayotoa mwelekeo wa kufikia malengo ya Jumuiya,” alisema Mary Makoffu, Mkurugenzi wa EAC anayeshughulikia Sekta ya Jamii wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kamati hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Mkutano huo, Agnes Sila kutoka Wizara ya Mambo ya Afrika Mashariki,Biashara na Utalii ya Kenya katika hotuba yake ya ufunguzi alisema Jukwaa la Katibu Mkuu lina umuhimu wa pkee katika suala zima la kuimarisha matangamano wa EAC.

“Jukwaa hili hutoa nafasi ya majadiliano ya moja kwa moja na Mtendaji Mkuu wa EAC katika harakati za kuimarisha mtangamano,” aliwaaambia wataalam kutoka nchi wanachama wa EAC.