Ugaidi Bungeni Dodoma

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi

*Wabunge waonywa, waambiwa wasipaki magari nje ya uzio, *Dk. Nchimbi asema ulinzi umeimarishwa kuliko kawaida

BUNGE limekumbwa na wasiwasi, baada ya kuwapo tetesi za shambulio la kigaidi katika viwanja hivyo. Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Bunge umechukua tahadhari kwa kuimarisha ulinzi katika jengo lote la Bunge pamoja na viunga vyake.

Hofu hiyo ilizidi kutanda baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, kutangaza hali hiyo juzi na kuwataka wabunge kuchukua tahadhari kuhusu usalama wa magari yao. Zungu alitoa tangazo hilo wakati wabunge wakiendelea na mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

“Waheshimiwa wabunge, wote mnaombwa kuanzia kesho (jana) kutoegesha magari yenu pembezoni mwa uzio unaozunguka ofisi za Bunge hapa Dodoma, badala yake, magari yaingizwe ndani ya uzio au yaegeshwe lango kuu upande wa barabara itokayo Dar es Salaam,” alisema Zungu kwa kifupi.

MTANZANIA ilifanikiwa kunasa ujumbe unaodaiwa ulitumika kusukuma ulinzi huo kuimarishwa, ambao unasomeka kama ifuatavyo.

“Kuna kikundi kina mkakati wa kufanya shambulio la bomu bungeni Dodoma na Msikiti wa Msamvu Morogoro ndani ya muda mfupi wakati vikao vya Bunge vikiendelea. NB: Muhimu Serikali kuchukua tahadhari haraka by raia mwema,” ulisema ujumbe huo.

Akizungumza na MTANZANIA nje ya ukumbi wa Bunge, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, alikanusha kuhusu taarifa za kuwapo kwa tishio lolote la kigaidi bungeni.

“Hakuna taarifa zozote tulizopata ambazo zinasema kuna dalili au viashiria vyovyote vya kigaidi au ulipuaji, lakini sisi kama Bunge tumeamua tu kuchukua tahadhari.

“Hii imetokana hasa na matukio ya hivi karibuni, Bunge ni taasisi muhimu, tumeona ni vema kuimarisha ulinzi badala ya kusubiri jambo baya litokee kisha tuanze kujutia, ni ulinzi wa kawaida tu ambao utakuwa endelevu,” alisema Joel.

Hata hivyo, akizungumza na MTANZANIA jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema ulinzi umeimarishwa katika eneo la Bunge baada ya kuwepo kwa taarifa za tishio hilo.

Kwa mujibu wa Dk. Nchimbi, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, limeimarisha ulinzi kuhakikisha usalama unaendelea kuwapo. Dk. Nchimbi alisema ulinzi utaendelea kuimarishwa katika eneo hilo kuliko wakati mwingine ambao umewahi kuwekwa na Bunge.

Kwa siku ya jana ulinzi ulikuwa umeimarishwa katika viwanja vya Bunge, ambapo kulikuwa na ongezeko la askari kanzu ambao walionekana wakizunguka maeneo ya Bunge kwa umakini. Mbali na askari hao, maeneo yanayozunguka Bunge ambayo yalizoeleka kuzagaa magari ya wabunge na yale ya wageni, jana hayakuonekana katika kuta za uzio wa Bunge kama sehemu ya kuimarisha ulinzi katika jengo hilo.

CHANZO: Gazeti Mtanzania