BENKI ya NMB Tanzania imedhamini ujenzi wa duka la Nafasi Art litakalotumiwa na watoto kujifunza mambo mbalimbali ambayo yanahusu sanaa ili kukuza vipaji walivyonavyo vya sanaa ili watakapokua waweze kuvitumia kutengeneza kipato. Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa duka hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke alisema udhamini huo ni sehemu ya malengo ya benki kuhakikisha inatenga pesa ambazo zitatumika kusaidia jamii.
“Benki yetu imekuwa ikitumia kitengo cha CSR kusaidia jamii kwa kutenga pesa kila mwaka ambazo zinatumika kusaidia jamii, tunaamini kuwa ujenzi huu utasaidia kuinua vipaji vya watoto ambao wanapenda sanaa ili wainue vipaji vyao,” alisema Ineke.
Naye Mkurugenzi wa Nafasi Art Space, Rebecca Correy aliishukuru NMB kwa uufadhili ambao wamewapa na kuwa banda hilo litawasaidia watoto wanaopenda sanaa kuonyesha vipaji vyao kwani kwa kipindi kirefu watoto wamekuwa wakikosa nafasi ya kushiriki kufanya kazi mbalimbali za sanaa lakini kwa sasa wataweza kuonyesha vipaji vyao.
Kwa upande wa mgeni rasmi kwenye halfa hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Joyce Hagu aliipongeza NAFASI Art Space kwa jitihada ambazo inazifanya za kukuza sanaa nchini na kuwa Serikali ya awamu ya tano itandelea kushirikiana nao.