Ufisadi Halmashauri ya Jiji Dar es Salaam

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi

HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam ilikiuka taratibu za utoaji wa zabuni ya kubomoa jengo lililokuwa ndani ya Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani kilichopo Ubungo (UBT), ambalo lilianguka mwanzoni mwa mwaka huu na kusababisha madhara kwa watu na mali. Januari 21 mwaka huu, watu wanne walijeruhiwa baada ya magari yao waliyokuwa wameyaegesha katika eneo la UBT kuangukiwa na ukuta, huku magari 24 na bajaji nne zikiharibika vibaya.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa Kampuni ya Makalla Contractors Ltd ndiyo iliyofanya kazi ya ubomoaji huo, lakini hakukuwa na mkataba wa kazi hiyo baina yake na Jiji la Dar es Salaam. Uchunguzi zaidi unaonyesha kuwa, licha ya kutokuwa na mkataba, Makalla Contractors Co. Ltd wamepeleka kwa uongozi wa jiji hilo madai ya Sh59, 615, 252 wakitaka walipwe kutokana na kazi hiyo.

“Makubaliano yalifanyika kwa mdomo na kazi ikaanza, hakukuwa na uitishwaji wa zabuni wala kufanyika taratibu zozote za kisheria, walipeana kazi hiyo kirafiki na baada ya jengo kubomoka ndipo walianza kuhaha jinsi ya kuwezesha kulipa fedha hizo,” kilisema chanzo chetu.

Katika moja ya nyaraka za kampuni hiyo kwenda Halmashauri ya Jiji, Kampuni hiyo ya Makalla inasema ilipewa kazi hiyo kutokana na gharama zake kuwa za chini na kwamba iliombwa kuanza kuitekeleza haraka kutokana na udharura wake kwa ahadi kuwa taratibu nyingine za kupewa LPO na mkataba zingefuata. Hata hivyo, taratibu za zabuni zinataka kazi itangazwe na hata kama kungekuwa na dharura ilipaswa kufuata utaratibu wa ‘single sourcing’ ambao ungewezesha kuchagua kampuni ya kutekeleza jukumu bila kuchelewa.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi ambaye ndiye mwenye dhamana ya kusaini mikataba kwa niaba ya jiji hilo alisema: “Sijawahi kusaini mkataba unaohusu kampuni hiyo unayoitaja (Makalla) na wala sijawahi kusaini mkataba kuhusu ubomoaji wa pale Ubungo.” Alipobanwa akitakiwa aeleze sababu za ubomoaji kufanywa bila yeye kuhusishwa alijibu: “Waulize watendaji wa Jiji, muulize mkurugenzi maana huo ni wajibu wa watendaji na siyo wajibu wa Meya, nilichokwambia ni kwamba mimi sijasaini mkataba wowote kuhusu suala hilo.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe alipoulizwa alisema hawezi kutoa taarifa kuhusu suala hilo kwenye vyombo vya habari.

“Wewe hizo taarifa umezipata wapi?… Mimi siwezi kukwambia mkandarasi gani aliyehusika, sitoi taarifa hizo kwenye vyombo vya habari… unazitaka za nini? Wananchi ndio wamekutuma uwatafutie taarifa? Wao wanatakiwa wasubiri huduma ikamilike, lakini siyo kumjua mkandarasi, kalipwa au hakulipwa,” alisema Kabwe.

Malipo kwa Mkandarasi
Wakati Kabwe akihoji maswali lukuki, habari zaidi zinasema ofisi yake imekuwa katika harakati za kuwezesha Kampuni ya Makalla kulipwa, na kwamba kinachokwamisha malipo hayo ni kutokuwapo kwa mkataba wa kazi. Fedha za ubomoaji kiasi cha Sh63 milioni zilitolewa na Ofisi ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) na kuhamishiwa kwenye akaunti za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, lakini imebainika kuwa kumekuwapo na harakati za fedha hizo kurejeshwa DART.

“Ofisi ya mkurugenzi inaendelea na mchakato wa kurejesha fedha hizo DART ili Kampuni ya Makalla ikalipwe huko maana ni ngumu malipo kufanyika hapa kwetu kwa sababu hakuna documents (nyaraka) za mkataba wa kazi, huwezi kulipa, sasa huko DART nao sijui watafanyaje,”kilidokeza chanzo chetu katika ofisi za Jiji. Hata hivyo, Ofisa Mwandamizi wa DART, Jack Meena alisema suala hilo linawahusu Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) na Halmashauri ya Jiji ambao ndiyo wamiliki wa kituo hicho.

“Sisi kazi yetu ni kuhakikisha eneo la mradi linakuwa tayari kwa ajili ya ujenzi. Kwa hiyo tulifanya tathmini na kulipa fidia na kumwachia mkandarasi,” alisema Meena.

Msimamizi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka katika Tanroads, Barakaeli Mmari alisema suala hilo linashughulikiwa na Halmashauri ya Jiji, hivyo waulizwe wenyewe.

“Ni kweli tunasimamia mradi wa mabasi yaendayo haraka, lakini suala la ubomoaji ni la Halmashauri ya Jiji. Wao ndio wanafahamu mkandarasi na kama alilipwa au hakulipwa,” alisema Mmari.

Sheria za Ubomoaji
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Kampuni ya Makalla iliandikiwa barua na Bodi ya Usajili wa Makadarasi (CRB), ikitakiwa kutoa maelezo ya kuhusika kwake katika kazi hiyo, pia vielelezo vilivyoonyesha jinsi kazi ilivyofanywa. CRB katika barua yake ya Mei 9, 2013 kwenda kwa Mkurugenzi wa Makalla Contractors Co. Ltd ambayo gazeti hili limeiona, ilitaka kampuni hiyo kuwasilisha mkataba wa kazi, majina ya wataalamu walioshiriki katika kubomoa jengo hilo na nyaraka za uthibitisho wa malipo yao.

Msajili wa CRB, Boniface Muhegi alikiri kwamba Kampuni ya Makalla imesajiliwa. “Halmashauri ya Jiji ndiyo waliomwajiri, ila kulipotokea malalamiko ndiyo tukawauliza (Jiji) wakakiri kwamba ndiye aliyefanya kazi hiyo,” alisema Muhegi na kuongeza:

“Mwanzoni kulikuwa na ubabaishaji. Tulipouliza tuliambiwa wenye magari waliambiwa wayaondoe kwanza… hilo ni tatizo la Jiji, lakini tutaichukulia hatua Kampuni ya Makalla kwa sababu imesababisha uharibifu wa mali za watu na kwa kutokuzingatia vigezo vya usalama kazini.” “Katika tathmini zetu tuna alama, kama zikifikia 60 au 70 tunatoa adhabu kulingana na kosa. Inaweza ikawa onyo, kusimamishwa kwa muda au kufutwa kabisa. Kwa kuwa hili ni kosa la kwanza tutaangalia vigezo vyetu,”alisema Muhegi.

Septemba 4, mwaka huu gazeti hili liliwasiliana na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Makalla Moseka ambaye awali alisema taarifa zote kuhusu suala hilo zinapaswa kutolewa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, lakini baadaye alimtaka mwandishi afike ofisini kwake kesho yake kwa maelezo zaidi.

Gazeti hili lilifika katika ofisi hizo, chumba namba tisa cha ghorofa ya 10 katika Jengo la Ushirika, Lumumba, lakini ofisi hizo zilikuwa zimefungwa, huku majirani zake wakisema kuwa ofisi hiyo imefungwa muda mrefu. Baada ya kumkosa, mwandishi alimpigia simu siku hiyo ya Septemba 5 ambapo Makalla alikanusha kwamba kampuni yake iliwahi kufanya kazi ya aina hiyo.

“Sikiliza bwana, mimi sikuhusika na kazi hiyo, inawezekana kuna watu walishafanya kazi kwenye kampuni hii, halafu wakaenda kufanya kazi kwa jina la kampuni yangu,” alisema Makalla.

Baada ya kubanwa zaidi, Septemba 7, Makalla aligeuka na kukiri kuhusika na kazi hiyo, huku akitaka mwandishi aonane naye Septemba 8. Alipotafutwa siku hiyo, alisema kwamba yuko msibani, hivyo kuahidi kwamba angekuwa tayari kuzungumza Septemba 10. Gazeti hili lilimtafuta juzi na jana, lakini mara zote alipopigiwa simu alikuwa akikata baada ya mwandishi kujitambulisha.

CHANZO: www.mwananchi.co.tz