RAIS Jakaya Mrisho Kikwete leo katika Ikulu ya Dar es Salaam amepokea Joho na Cheti cha Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Sheria yaani Doctor of Laws, Honoris Causa kutoka kwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam UDSM.
Tayari Rais Kikwete alishatunukiwa shahada hiyo katika mahafali ya 41 ya UDSM yaliyofanyika Octoba, mwaka 2011 na leo hii UDSM. Rais Kikwete ametunukiwa shahada hiyo kwa sababu ya utumishi wake uliotukuka kwa Umma wa Watanzania na jamii nyingine zilizo nje ya mipaka ya Tanzania.
Akisoma maelezo mafupi kabla ya kumkabidhi cheti na kumvisha Joho, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma Prof. Florens Luoga amesema Shahada hii ya juu kabisa miongoni mwa tuzo zinazotolewa na UDSM, kulitokana na uamuzi uliofanywa na Seneta na kuridhiwa na Baraza la Chuo.
”Seneta ilizingatia busara, wema na Umakini uliodhihirika katika maisha yako yote ya uongozi, tangu ulipokuwa kijana hadi ulipofikia ngazi ya juu kabisa ya uongozi katika nchi yetu,”ameeleza.
Rais Kikwete ameshukuru kwa Shahada hiyo na kueleza nia yake ya kuendelea kukisaidia Chuo Kikuu hicho ambacho ndiyo chuo Kikuu kikongwe hapa nchini.
“Nitaendelea kutoa mchango wangu katika Chuo chetu ambacho ndiyo Kikubwa hapa nchini kwa lolote ambalo naweza kulifanya kwa ajili ya Chuo sasa na hata baadaye” Rais ameahidi na kupata maelezo kutoka kwa Makamu wa Mkuu wa Chuo Prof. Rwekaza Mukandala ya jinsi mchango wake umechangia katika kutengeneza dira ya UDSM.
Prof. Mukandala amesema baadhi ya mchango mkubwa wa Rais katika Chuo hicho ni kuanzishwa kwa shule ya Madaktari na masomo ya sayansi ya Kilimo ambayo yanatarajiwa kuanza rasmi mwezi Octoba mwaka huu. Katika hatua ingine Rais Kikwete pia amepokea hundi yake ya Bima ya maisha (Flexi Provider) ambayo amekuwa nayo kwa kipindi cha miaka 9.
Akimkabidhi hundi hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima Tanzania Limited (NIC) Bw. Sam Kamanga amesema uwepo wa Rais kama mteja wa NIC imesaidia kukuza uelewa na shughuli za shirika hilo.
“Kitendo cha Serikali kukatia Bima mali zake na taasisi zake, kumeongeza uwezo wa kifedha wa shirika na soko la Bima” amesema na kuwataka watu binafsi, taasisi mbalimbali na mashirika ya kiserikali kukata Bima kwa ajili ya maendeleo na akiba ya baadaye. Rais Kikwete ameitaka NIC kuongeza juhudi katika kuhamasisha na kuelimisha watanzania umuhimu na manufaa makubwa yanayopatikana kutokana na Bima.