Magreth Kinabo- MAELEZO, Dar es Salaam
SERIKALI imesema mapato yanayopatikana kwenye Kivuko cha Magogoni yameongezeka toka sh. milioni sita hadi kufikia sh. milioni tisa kwa siku baada ya kufanyika hatua mbalimbali ikiwemo kuingia mkataba na kampuni ya ulinzi ya SUMA JKT.
Aidha serikali imetangaza ongezeko la viwango vya nauli katika vivuko vyote nchini kuanzia Januari Mosi, mwaka huu, ambapo kwa upande wa abiria watu wazima bei zimeanzia sh.200 hadi sh.300 kulingana na maeneo.
Katika bei hizo, watoto chini ya miaka 14 watalipa sh. 50, na wanafunzi waliovaa sare na wenye vitambulisho hawatatozwa nauli kabisa utaratibu ambao ulikuwa ukitumika katika vivuko vyote nchini.
Amesema bei za vyombo vya usafiri zimeanzia sh. 500 hadi 80,000 kulingana na aina ya chombo cha usafiri, uwezo wa kubeba abiria na mizigo, uzito na maeneo. Viwango vya nauli hizo vitabandikwa katika sehemu zote za vivuko, hivyo wananchi kutakiwa kuvifuata.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli alipokutana na wanahabari kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara hiyo jijini Dar es Salaam. Akizungumzia kupanda kwa mapato ya vivuko amesema imetokea baada ya Serikali kupambana na vitendo vya watumishi wasio waaminifu kuanzia Julai mwaka jana.
Waziri Magufuli alisema Wakala wa Ufundi na Umeme (TAMESA) katika kipindi hicho iliamua kubadili wakata tiketi na kuajiri wengine, ambapo imeondoa askari wa kuajiriwa na wakala badala yake kuingia mikataba na kampuni ya ulinzi ya SUMA JKT ambayo ndiyo inayotumika kufanya kazi hiyo kwa sasa.
“Wizara itaendeleza hatua hizi kwa lengo la kubana uvujaji wa mapato na matumizi yasiyo ya lazima kwa vivuko vyote nchini,” alisisitiza huku akiongeza kuwa wanampango wa kuanzisha tiketi za elektroniki ili kutumia mbiu za kisasa katika kudhibiti suala hilo.
Akizungumzia kuhusu ongezeko la nauli za vivuko alisema Wizara yake kupitia TAMESA imeongeza viwango hivyo ili kuendana na gharama za uendeshaji mabazo ni kuongezeka kwa misharahara ua watumishi serikalini kwa zaidi ya asilimia 100, mafuta zaidi ya asilimia 400, vipuri na kodi, ikiwemo bei kwa ujumla.
Waziri Magufuli alivitaja viwango hivyo vya nauli kwa kivuko cha Magogoni, Kigamboni na Alina ni sh. 200 badala ya sh. 100, Pangani bei ni sh. 200, wakati awali ilikuwa ni hivyohivyo, ingawa umbali wake hauzidi wa Magogoni. Ilagala – Kajeje, Kasharu -Buganguzi, Ilunga – Kipigu bei ni sh. 200 awali ilikuwa sh. 100 na Kilombero- Ulanga na Utete – Mkongo bei imebakia kuwa ni sh. 200.
Kivuko cha Kigongo – Busisi, Kisorya – Rugezi, Nyakaliro – Kome na Musoma – Kinesi vyote bei ni sh. 400 badala ya sh. 300 iliyokuwa ikitozwa hapo awali. Alisema kivuko cha Kilambo – Namoto bei ni sh. 500, ambapo awali iliuwa hivyohivyo Pwani – Msanga Mkuu sh. 300, Rusumo – Nyakiziba na Itungi ni sh. 200. Bugorola- Bwisya sh. 800 wali ilikuwa sh. 500.
Vivuko vya Chato – Ikumbaitale – Izumacheli- Nkome ni imebakia kuwa sh. 3000 na kituo hadi kituo 800 awali ilikuwa sh. 500 na Chato – Bukondo – Nsenga- Muharamba imebakia sh. 2000 ,wakati kituohadi kituo sh. 800 awali ilikuwa sh. 500.
Alisema upandishaji wa nauli hizo umefanywa kwa kuzingatia taratibu za kisheria na kutangazwa kwenye gazeti la serikali toleo namba 367 Aprili mwaka jana, hivyo kulingana na sheria za uendeshaji wa vivuko vya serikali sura ya 173 kifungu 11 mwenye mamlaka ya kupanga nauli ni Waziri mwenye dhamana na vivuko vya serikali.
Waziri Magufuli alisema bei za vivuko vingine zimepandishwa zaidi ya mara mbili tangu mwaka 1997, lakini cha Kigamboni kimekuwa kikitoza bei ya sh. 100 kwa mtu mmoja. Waziri Magufuli alisema wanampango wa kuanzisha kivuko kingine kutoka Feri hadi Bagamoyo na mtoni kijichi ili kupunguza msongamano kwa kutumia bahari.