Na Mwandishi Wetu
UCHAGUZI wa viongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi Tawi la Vigaeni, Kata ya Ndugumbi Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, unafukuta kutokana na kudaiwa kuwa na mchezo mchafu.
Uchaguzi huo bado haujajulikana utafanyika lini, ingawa zoezi la urudishwaji wa fomu za wagombea ulishakamalika tangu Jumapili iliyopita. Baadhi ya wanachama wa jumuiya hiyo, wamesema zoezi la uchaguzi wa viongozi wao unaonekana kuwa katika zengwe kutokana na kurudishwa kwa majina ya wagombea.
Wanachama hao walidai kuwa kurudishwa kwa fomu ya mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Tawi la Vigaeni (jina linahifadhiwa) kunatokana na kutakiwa kuwepo kwa majina ya ‘wateule’ wao.
“Unajua kuwa kuna mambo ambayo hata hatuyaelewi kabisa, kwa mfano jina la mgombea wa nafasi ya mwenyekiti limetakiwa kurudi kisa liko moja, na mgombea hawezi kuwa peke yake,” alisema mmoja wa wanachama hao.
Wakizungumza kwa nyakatio tofauti, wanachama wa tawi hilo wamedai kuwa kuwepo kwa tofauti ya jina moja kuondolewa, huku nafasi ya katibu ikiwa na mgombea mmoja, sambamba na nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu Kata. lilipowasiliana na Ofisi ya Katibu Mkuu wa Tawi la Vigaeni, lilijibiwa kuwa katibu huyo hayupo kazini kutokana na kusumbuliwa na maradhi.
Mmoja wa wafanyakazi wa ofisi hiyo ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Shida, alisema yeye si msemaji, na kumtaka mwandishi kuwasiliana na katibu, ambaye kwa wakati huo alidai yuko nyumbani kwake na anaumwa.
Tawi hilo linadaiwa kufukuta kutokana na baadhi wa wagombea kuwekewa kauzibe kwa vigezo vya kutokuwa wakazi, kitu ambacho kinavumishwa ikidai kuna mbinu kwa baadhi ya watu kutakiwa kushika baadhi ya nyadhifa.
Hata hivyo, wagombea wote wa nafasi tofauti walizoomba wamefanyiwa usaili jana, huku nafasi ya mwenyekiti ikitakiwa kutafutiwa mpinzani, baada ya awali kuwasilishwa jina moja hadi siku ya mwisho ya kurudisha fomu iliyokuwa Mei 6.