MAHASIMU wa kisiasa nchini Zimbabwe, Rais Robert Mugabe na Waziri Mkuu wake, Morgan Tsvangirai wamenadi sera zao kwa malengo ya kulikwamua taifa hilo kiuchumi, ili kuwavutia wapiga kura wao kabla ya Julai 31.
Kwa mujibu wa tathmi ya shirika la habari la Ufaransa AFP mahasimu hao waliendelea kujinadi mwishoni mwa wiki ikiwa zimebaki takribani wiki mbili na nusu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa taifa hilo, unaotarajiwa kuifikisha kikomo serikali ya mizengwe iliyolazimishwa kuundwa kutokana na uchaguzi wenye vurugu wa mwaka 2008.
Akizungumza katika kampeni zake katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini ya almasi kwa upande wa mashariki, Tschangirai alisema; “Chaguo ni rahisi sana, ni kati ya serikali iliyoshindwa kwa zaidi ya miaka 33 na ahadi mpya ambazo ziko wazi kabisa.” Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 61 alizungumza katika mji wa Mutare akimtolea mfano rais Mugabe kuwa mwenye kutaka kuhodhi madaraka.
Mugabe mwenye umri wa miaka 89, akiwa amevalia kanzu nyeupe huku ameshika biblia mkononi alijitokeza mbele ya maelfu ya wafuasi wake waliokusanyika katika eneo la kanisa moja huko mjini Marange, umbali wa kilometa 200, mashariki mwa mji mkuu Harare.
Akinukuliwa na AFP kiongozi huyo mkongwe barani Afrika alisema; “Tulifanya makosa 2008 kumchagua mtu ambae anapenda Wazungu. Kumpigia kura mtu ambae anataka kuwarejesha wazungu na ambae anafikiri haiwezekani kuwepo kwa maendeleo nchini Zimbabwe bila kuhusishwa watu hao” Alisema rais Mugabe.
Katika kunadi sera zake kiongozi huyo mkongwe alilenga masuala ya uzawa, au sera za uzawa na kuwawezesha watu weusi akisema kwamba Zimbabwe lazima imiliki sehemu kubwa ya rasilimimali yake. Kwa upande wake Tsvangirai ameahidi kurekebisha uchumi, kufufua viwanda na kuvutia uwekezaji kwa lengo la kupanua wigo wa ajira kwa vijana nchini humo.
Akizungumza mbele ya maelfu ya wafuasi waliovaa fulana nyekundu zenye picha yake. Tsvangirai ameahidi kufanikisha uwazi katika uchimbaji wa madini ya almas. Nikimunukuu kiongozi huyo wa upinzani hapa alisema; “Wapi zinapokwenda fedha za almas? Tunafahamu tukipata fedha zote kutoka katika madini hayo tunaweza kuunda ajira mpya laki moja.
Alisema katika mkutano wake wa kampeni uliyofanyika katika uwanja wa Mutare, uliyopo kilometa 250 mashariki mwa Zimbabwe. Aliongeza kusema kama mapato yote kutoka katika madini hayo yangefika moja kwa moja katika mikono ya serikali wangaliweza kulia walimu na wanajeshi na sio kama ilivyo sasa ambapo mapato hayo yanawanufaisha watu wachache. Kama atapewa ridhaa ya Wazimbabwe kuongoza taifa hilo Tsvangirai ameahidi kupitia upya mikataba yote katika sekta ya madini kwa kuwa ya sasa inatoa mianya ya kuendelea kwa vitendo vya rushwa.
Aidha katika kampeni yake rais Robert Mugabe amepinga ndoa za jinsia moja kuwa zinakwenda kinyume na utamaduni wa Afrika na kuikosoa vikali kauli ya rais Obama barani wakati alipozulu Afrika kuhimiza waafrika kuheshimu haki za mashoga. Mugabe alisisitza kauli yake hiyo kwa kusema ndoa ni ya mwanamke na mwanaume ambapo matunda yake ni kuzaliwa watoto.
Katika uchaguzi uliyopita Zimbabwe iligubikwa na visa vya umwagikaji damu. Tsvangirai alijiondoa katika kinyanganyiro hicho pamoja na cha mwaka 2008 pamoja na kuibuka na ushindi katika duru ya kwanza. Uchaguzi wa mwezi huu unatajwa kuwa wenye kuweza kuifikisha serikali ya mseto nchini humo ambayo imesababisha kudidimia kwa uchumi.
-DW