Na Margareth Chambiri – Dar es Salaam
MKURUGENZI wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani amesema jambo kubwa ambalo watanzania wanapaswa kujifunza kutokana na Uchaguzi wa Marekani uliomalizika hivi karibuni ni kwa wananchi kuheshimi mifumo ya Uchaguzi.
Mkurugenzi Kailima ametoa kauli hiyo ikiwa ni tathimi yake kuhusu uchaguzi huo wa Marekani na namna ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakihoji kuhusu ucheleweshaji wa kutangaza matokeo ya uchaguzi unaofanywa na Tume ikilinganishwa na ilivyofanyika nchini Marekani.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na Kituo cha Redio cha Clouds FM, Kailima amesema siyo sahihi kulinganisha uchaguzi wa Marekani na Tanzania, akitolea mfano sekta ya mawasiliano ambayo ni muhimu katika kusafirisha vifaa na taarifa mbalimbali za uchaguzi inavyokabiliwa na changamoto.
Amesema watanzania na hasa Wapiga kura wengi wanaishi maeneo ya vijijini ambayo baadhi yake hayafikiki kwa urahisi na kwamba haiwezekani Tume ikatangaza matokeo bila kuhakikisha kuwa kila kura imehesabiwa ikiwemo ya yule mwananchi wa kijijini.
Amebainisha kuwa yapo mambo ya msingi ambayo watanzania wanapaswa kujifunza kutokana na Uchaguzi wa Marekani, kubwa ikiwa ni hatua ya kuheshimu mifumo ya Uchaguzi sambamba na Mamlaka zinazosimamia chaguzi hizo.
Ametolea mfano wa uvumilivu katika kusubiri matokeo na Wagombea kuheshimu matokeo yanayotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa sheria kwani hata pale ambapo anayeshindwa hakuridhika bado anaweza kupinga matokeo kwa kufuata taratibu zilizopo kisheria.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi inakamilisha Mwongozo wa Utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura wa 2015-2020 ili iweze kuzishirikisha Asasi za Kiraia, Taasisi au Vikundi mbalimbali vya Watu wanaotaka kutoa Elimu hiyo.
Kwa mujibu wa Bwana Kailima Tume imo katika hatua za mwisho za kupitia Rasimu ya Mwongozo wa Elimu ya Mpiga Kura kwa ajili ya kuupitisha uweze kutumiwa na Wadau mbalimbali wa Uchaguzi. Amesema pamoja na hatua ya Tume ya kuanza kutoa Elimu ya Mpiga Kura mapema kuliko ilivyozoeleka na wananchi, inakusudia kupanua zaidi wigo wa utoaji wa Elimu hiyo kwa kuwashirikisha wadau wengi zaidi wakiwemo Viongozi wa Dini.
Bwana Kailima amesema Tume kupitia kwa Mwenyekiti wake Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Damiani Lubuva baadaye mwezi huu itatoa taarifa rasmi kwa ajili ya kuzialika Taasisi na Asasi za Kiraia zinazotaka kutoa Elimu ya Mpiga Kura kuwasilisha maombi yao kwa ajili ya kupatiwa kibali rasmi cha kutoa Elimu ya Mpiga Kura.
Aidha Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi amevitaja vigezo vya kupatiwa kibali kwa ajili ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura kuwa ni pamoja na Cheti cha Usajili, Asasi au Taasisi kuwa imefanya kazi nchini kwa kipindi kisichopungua miezi sita pamoja na kuwasilisha majina ya watendaji wa juu wa Taasisi au Asasi husika.
Akizungumzia kuhusu tathmini ya zoezi hilo linaloendelea kufanywa na Tume yake, Bwana Kailima Halmashauri amesema limekuwa na mafanikio makubwa na anaamini kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Uchaguzi kutawezesha wananchi wengi kufikiwa na Elimu hiyo na kwamba Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 hakutakuwa na malalamiko na badala yake zoezi la uchaguzi litakuwa rahisi.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi tayari imeanza utekelezaji wa zoezi la Utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura ambapo imeshiriki katika maonesho mbalimbali yakiwemo ya Biashara ya Kimataifa na yale ya Wakulima pamoja na kutembelea na kutoa Elimu ya Mpiga Kura katika shule kadhaa za Sekondari hapa nchini.