Ubunifu wa BRN Wavutia Wawekezaji Sekta Binafsi

Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima.

Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima.


Na Mwandishi Wetu

MKUTANO wa kwanza wa aina yake ulioandaliwa na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) umefanikiwa kuwakutanisha mahali pamoja wawekezaji wakubwa kutoka mataifa mbalimbali ili kujionea fursa za uwekezaji katika miradi mbalimbali iliyopewa kipaumbele katika Mpango huo.

BRN ni Mpango ulioanzishwa na Serikali ya Tanzania tangu Julai mosi, 2013 kwa lengo la kuchagua sekta chache za kipaumbele na kuweka mfumo madhubuti unaoweka malengo na muda wa utekelezaji wa kila mradi huku mawaziri husika wakiwa wamesaini mikataba ya utekelezaji na Rais.

Mkutano huo wa kuwaweka pamoja wawekezaji wote na kupata fursa ya pamoja ya kuelezwa fursa zilizopo katika miradi ya kipaumbele ya BRN ni ubunifu mkubwa unaoonesha nia na utayari wa Serikali ya Tanzania katika kuruhusu ushirikiano na sekta binafsi.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wawakilishi kutoka mabenki na taasisi nyingine kubwa za kimataifa na kufunguliwa na Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, sehemu kubwa ya wawekezaji hao walivutiwa na ubunifu huo wa BRN na kueleza jinsi walivyopewa nguvu ya kushirikiana na Serikali.

Kupitia Kurugenzi yake ya Ukusanyaji wa Mapato, BRN imekuwa ikichagiza kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya umma ikiwemo pia kusaidia mabadiliko ya kisera na kisheria ili kuimarisha uhusiano huo. Mikutano kama hii na wawekezaji ni jambo litakalokuwa la kila mara, anasema Lawrence Mafuru kutoka BRN.

Tukio la Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Katibu Mkuu wake, Dk. Shaaban Mwinjaka kukaa kwa siku nzima katika mkutano huo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa kuungana na timu yake katika dawati la kusikiliza wateja vilikuwa moja ya vivutio kwa wawekezaji wengi katika kupata imani juu ya utayari wa Serikali kuwashirikisha katika uwekezaji.

“BRN inaleta ubunifu na utamaduni wa kuweka vipaumbele katika miradi kuitekeleza kwa wakati lakini pia kuvutia wawekezaji binafsi kushirikiana na Serikali. Hii ni sehemu ya tofauti kubwa ambayo BRN inaeleta katika utumishi wa umma nchini Tanzania,” alisema Bw. Mugisha Kamugisha, Mkurugenzi wa Mipango katika Ofisi ya Rais-Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (PDB) inayosimamia BRN.