- *Madereva wa mabasi ya mikoani wagoma
- *Abiria wataabika, FFU watembeza virungu
- *Kova azomewa, aambiwa aache siasa
-
VURUGU kubwa za aina yake, ziliibuka jana katika Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani kilichopo Ubungo Dar es Salaam, baada ya madereva wa mabasi kugoma wakilalamikia mikataba ya ajira.
Sambamba na malalamiko hayo, wadereva hao waligoma kwa sababu hawaridhishwi na utendaji kazi wa Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kuwa askari wa kikosi hicho wamekuwa wakiwakamata na kuwadai rushwa pindi wanapofanya makosa ya barabarani.
Miongoni mwa mikoa iliyolalamikiwa na madereva hao ni Iringa na Mbeya ambayo inaelezwa kukithiri kwa rushwa miongoni mwa askari wa kikosi hicho.
Kutokana na vurugu hizo zilizodumu kwa zaidi ya saa sita, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walimwagwa kituoni hapo ili kurejesha hali ya amani iliyotaka kutoweka kwa kuwa baadhi ya abiria walichachamaa na kutaka warudishiwe nauli au madereva wasitishe mgomo.
Hali katika kituo hicho ilikuwa mbaya zaidi karibu kila kona huku akina mama na watoto wakitaabika baada ya kutokuwa na uhakika wa usafiri kuelekea walikokuwa wakienda.
Abiria walijazana kila kona, wengine walikuwa katika mabasi waliyotarajia kusafiri nayo, wengine walikuwa wakitembea huku na kule na wengine walikuwa wamesimama mbele ya vituo viwili vya polisi vilivyo kituoni hapo.
Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya madereva waliokuwa wamegoma walilazimika kukaa kwenye baadhi ya baa na kupata vinywaji wakisubiri hatima ya mgomo wao.
Vyoo vilivyopo kituoni hapo vilifurika watu na mara zote watu walikuwa wamepanga foleni katika vyoo vya kike na vya kiume huku kila mmoja akisubiri zamu kwa ajili ya kujisitiri.
Katika vyumba vya vyoo, abiria walikuwa wakifokeana pindi mmoja wao anapongia chooni na kuchelewa kutoka baada ya kujisitiri.
Kwa upande wa maduka na hoteli msemo wa kufa kufaana jana ulichukua nafasi yake kwani wauzaji wa maeneo hayo walikuwa ‘bussy’ wakati wote kwa kuwa walikuwa wakihudumia wateja masaa yote, wengi wao wakiwa ni abiria waliokuwa wamekwama kutokana na mgomo huo.
Pamoja na hali hiyo, vurugu kubwa zaidi zilitaka kutokea baada ya kundi la abiria kutaka kuvamia ukumbi wa mikutano walimokuwa viongozi wa serikali wakijadili namna ya kutatua mgomo huo.
Miongoni mwa waliokuwa katika ukumbi huo ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, viongozi wa Umoja wa Madereva, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga na maofisa kadhaa wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA).
Wakati viongozi hao wakiendelea na kikao, nje ya ukumbi huo kulikuwa na kila dalili ya amani kutoweka kwa kuwa kundi la abiria lilitaka kuvunja mlango wa ukumbi na kuingia ndani ili kupambana na waliokuwa ukumbini humo.
Pamoja na sababu zingine, abiria hao walikuwa wakilalamikia kikao hicho kwa kile walichosema kuwa hakiwasaidii chochote kwani shida yao ilikuwa ni kusafiri wala siyo vikao.
Baada ya kuwapo dalili mbaya, Kamanda Kova alitoka nje ya ukumbi ili kuwatuliza abiria hao lakini aliambulia maneno ya kashfa na matusi kutoka kwa abiria hao ambao walimzomea na kumwambia aache siasa badala yake ashughulikie mgomo huo.
Tukio hilo lilisababisha FFU kuingilia kati na kulazimika kutembeza virungu na kuwatawanya abiria hao. Abiria walipoona hali hiyo, walitimua mbio kisha wakasimama na kujibu mapigo kwa kuwarushia mawe na chupa za maji askari hao.
Akizungumzia tukio hilo, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva, Yusuf Mgumba, alisema yeye na madereva wenzake wanawataka wamiliki wa mabasi wawape mikataba ya ajira ili wawe wanalipwa mshahara wa Sh 350,000 kwa mwezi na posho za safari.
“Tumegoma kwa sababu tunataka mishahara na pia ‘matrafiki’ wa mikoa ya Mbeya na Iringa waache kutunyanyasa kwa sababu wakitukamata kwa visingizio vya mwendo kasi, wanatuomba rushwa au kutuandikia faini ya Sh 100,000 hadi 250,000.
“Tunataka pia tukatiwe bima na kuwekewa akiba ya uzeeni kutokana na mishahara yetu baada ya kukatwa kodi ya Serikali kwa sababu kazi tunazozifanya ni za hatari kwani wakati wowote mtu unaweza kupoteza maisha.
“Malalamiko yetu siyo hayo tu, tunataka pia uongozi wa jiji utupatie sehemu ya kuweka ofisi ya chama chetu ndani ya kituo cha mabasi na pia tunataka watuongeze muda wa kubadilisha leseni za udereva,” alisema Mgumba.
Kamanda Mpinga alisema malalamiko ya madereva hao ameyapokea na atayafanyia kazi ili kuondoa usumbufu kwa abiria kwa siku zijazo.
“Inaonekana kero nyingine ni kwa ‘traffic’, sasa nimetoa maelekezo kwa ma-RTO wa Mikoa ya Iringa na Mbeya, hawa wako chini yangu, nimewataka washughulikie malalamiko ya rushwa na kuhusu suala la muda wa utoaji leseni, tumeshalipeleka kwa Waziri wa Uchukuzi, analifanyia kazi,”alisema Kamanda Mpinga.
Naye Kamanda Kova aliwaambia viongozi wa madereva hao, kwamba amejifunza mambo mengi sana kutokana na mgomo huo na kuwataka madereva wasitishe mgomo kwa kuwa ataunda kamati itakayoshughulikia matatizo yao.
“Tumeamua kulibeba jambo hili kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, mkiwa na matatizo msisite kutujulisha kabla hamjaamua jambo kama hili kwa sababu nyie ni viongozi kama tulivyo sisi.
“Jaribuni kuwa na moyo wa huruma, miongoni mwa wasafiri waliokwama hapa wamo watoto na wagonjwa na ili kulitatua hili tutakuwa na kikao keshokutwa (kesho) ili kujadili suala lenu, yote tutayazungumza na naomba mniamini.
“Nitahakikisha mikataba halali inatolewa na waajiri wote, lazima watoe mikataba halali badala ya mikataba feki inayowanyima haki madereva,” alisema Kamanda Kova.
Kaimu Mkurugenzi wa SUMATRA, Ahmad Kilima, aliwataka madereva kuwa makini na mikataba yao ili iwe na vipengere vinavyolinda haki zao.
Pamoja na hali hiyo, hatimaye mgomo ulisitishwa na basi la kwanza kuondoka kituoni hapo lilikuwa ni Chakito lenye namba za usajili T 305 ANH linalofanya safari kati ya Dar es Salaam na Arusha. Basi hilo liliondoka saa saba mchana badala ya saa 12 asubuhi.
Hata hivyo, pamoja na baadhi ya madereva hao kudaiwa kulewa, wengi wao ndiyo walioendesha mabasi hayo bila kujali mazingira ya usalama wa abiria wao.
Chanzo: Gazeti la Mtanzania