Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kushirikiana na klabu maarufu duniani ya mpira wa miguu ya Real Madrid ya Hispania, leo imeendelea na zoezi lake la usajili wa vijana walio na umri wa chini ya miaka 14 watakaofanyiwa majaribio kwa ajili ya kujiunga na kituo cha michezo cha NSSF-REAL MADRID SPORTS ACADEMY katika uwanja wa Karume mjini Dar es Salaam, huku idadi ya vijana wanaojisajili ikiongezeka.
Mchakato huo wa usajili ulianza Oktoba 14 lakini leo idadi ya vijana wanaojitokeza ikiongezeka kwa kasi ambapo jumla ya vijana 257 wamejitokeza kuandikiswa katika viwanja vya karume jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia zoezi hilo kwa wanahabari katika viwanja vya Karume, Kaimu Meneja Kiongozi wa Idara ya Uhusiano na Huduma kwa Wateja, Salim Khalfan Kimaro wa NSSF, alisema uandikishaji wa vijana katika zoezi hilo leo umeongezeka kutokana na idadi kubwa kujitokeza kuandikishwa.
Akitoa ufafanuzi zaidi Kimaro alisema watoto walengwa ni wale waliozaliwa kuanzia Januari, 2001 hadi Disemba, 2003 na ili mtoto aandikishwe anatakiwa kuambatana na mzazi wake au mlezi anayetambulika kisheria na aje na nyaraka za uthibitisho wake kuwa ni mlezi halali kwa kuonesha vithibitisho vya kisheria.
“…Kwa mtoto husika, aje na cheti halisi cha kuzaliwa na kopi yake pamoja na picha ndogo (passport size) zenye rangi ya bluu. Zoezi hili litaendelea tena wiki ijayo tarehe 21 na 22 Februari ambapo baada ya hapo michezo ya majaribio itaanza wiki zinazofuatia,” alisema Khalfan Kimaro.
Aidha aliongeza kuwa watoto 30 watakao fuzu kuingia katika kituo cha mafunzo wataandaliwa mazingira kuhakikisha wanaendelea kupata elimu bila kikwazo chochote. Alisema Shirika la NSSF linatoa wito kwa wazazi na walezi kujitokeza kuwaleta watoto wao kujiandikisha ili kuendeleza vipaji vyao kwa fursa iliyotolewa.