U-‘Busy’ wa Wazazi Kibiashara Unavyoathiri Taaluma kwa Wanafunzi

Moja ya mazoko ya mzunguko (magulio) yaliokoa Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro

Na Mwandishi Wetu, Rombo

LICHA ya kuwepo kwa shule za msingi na sekondari kwa Mkoa wa Kilimanjaro ambazo kwa kiasi fulani zinakidhi mahitaji, bado kuna changamoto kadha wa kadha ambazo zinaathiri maendeleo ya kitaaluma kwa baadhi ya maeneo. Wilaya ya Rombo ambayo ni moja ya wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na changamoto za kipekee kitaaluma hasa elimu ya sekondari.

Wilaya hii imefanikiwa kuwa na shule nyingi za sekondari hasa zile za Serikali licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa katika uendeshaji wa shule hizi. Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wadau wa elimu wilayani Rombo, kuna jumla ya shule za Sekondari 48; yaani shule zinazomilikiwa na Serikali 41 huku zile za binafsi zikiwa saba tu.

Tofauti na maeneo mengine ya Tanzania idadi kubwa ya wazazi wilayani Rombo wana mwamko wa kuwapeleka watoto wao shule kupata elimu ya sekondari mara baada ya elimu ya msingi. Hatua hii pekee ya kumpeleka sekondari mtoto ni kutambua umuhimu wa elimu kiasi fulani kwa mtoto. Wapo pia wanaojitahidi na hata kulipa michango na mahitaji kwa wakati japo si wote.

Lakini kumpeleka mtoto shule na kutomfuatilia anafanya nini wakati gani na hata anaporudi nyumbani baada ya shule haitoshi. Uchunguzi mdogo uliofanyika katika baadhi ya maeneo ya mpakani mwa Tanzania na Kenya katika ndani ya Wilaya ya Rombo, yakiwemo maeneo ya Holili, Tarakea na Rongai imebaini licha ya baadhi ya wazazi kuwa na mwamko wa kuwapeleka sekondari watoto wao hawafuatilii maendeleo yao kabisa.

Moja ya masoko ya mzunguko (magulio) yalioko wilayani Rombo, Kilimanjaro.


Hali hii imesababisha wanafunzi hao kujihusisha na shughuli nyingine zaidi ya elimu za kutafuta fedha (biashara). Maeneo haya yapo mpakani sehemu ambazo zinashughuli nyingi za kibiashara na kazi ndogo ndogo za kufanya. Uchunguzi umebaini wapo wanafunzi ambao hufanyabiashara na kazi za vibarua ndogo ndogo huku wakiendelea na shule jambo ambalo linaathiri maendeleo yao kitaaluma na eneo zima.

Wapo wanafunzi wa sekondari ambao hufanya kazi za kuendesha pikipiki za abiria maarufu kama bodaboda mpakani na huku wakiendelea na shule, wapo pia ambao hufanya vibarua vya kubeba mizigo na hata kulimishwa kwenye mashamba hasa eneo la Kenya na kulipwa ujira wa siku. Shughuli hizi za utafutaji kipato zinapowanogea wengine huacha kabisa shule na kuendelea za shughuli za utafutaji kipato.

Wasichana wao hukimbilia kufanya kazi za ndani hasa kwa wenyeji wa Kenya na pia kufanya kazi za uuzaji vinywaji baa. Mji wa Loitokitoki uliopo mpakani kabla ya kuingia nchini Kenya ndio wenye idadi kubwa ya biashara na shughuli kama hizi ambazo hufanywa na wasichana wengine wakiwa wamekimbia shuleni ama baada ya darasa la saba bila kujali kama amechanguliwa kuendelea au kuishia mnjiani kutokana na uangalizi mdogo ki-malezi.

Ramadhan Ally ni mmoja wa wakazi wa Tarakea wilayani Rombo, anasema baadhi ya wanafunzi huamua kujiingiza kwenye shughuli za utafutaji kipato kutokana na usimamizi mdogo wa wazazi/walezi wao. “Wapo wazazi ambao wamewaacha watoto wao chini ya uangalizi wa bibi au babu wao wapo ‘busy’ kibiashara nchini Kenya, wapo wazazi wengine huwashirikisha watoto wao kufanya vibarua vya mpakani ili kukuza kipato cha familia…sasa hali kama hii inamfanya mtoto asione umuhimu wa shule na wakati mwingine baadae uamua kuacha kabisa shule,” anasema Ally.

Anaongeza kuwa wapo baadhi ya wazazi hawawatimizii mahitaji ya shule watoto wao hivyo watoto kuamua kutafuta chochote wenyewe. Hili huwenda likawa na ukweli, uchunguzi uliofanyika katika sekondari za Tanya, Nduweni, Ngaleko, Urauri na Mbomai umebaini muitikio wa ulipaji wa ada na michango mingine kwa wazazi/walezi ni mdogo sana kwa wazazi. Kiujumla madeni ni mengi dhidi ya wanafunzi.

Moja ya masoko ya mzunguko (magulio) yalioko wilayani Rombo, Kilimanjaro.


Venance Mramba ni Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Sekondari ya Nduweni, katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya anakiri mwamko mdogo wa waza/walezi kwa ulipaji ada na michango mingine shuleni hapo. “…Ukweli hapa madeni ya wanafunzi ni mengi ikiwemo ada na michango mingine…,” anasema Mramba.

Victus Kiwango ni Mkuu wa Sekondari ya Tanya iliyopo wilayani Rombo maeneo ya mpakani, anakiri pia mwamko mdogo wa wazazi kuchangia ada na michango mingine katika shule yake, anaongeza kuwa wapo wanaodiriki kusema kuwa uwezo wao kiuchumi ni mdogo wa ulipaji ada na michango mingine. 

Hata hivyo kwa upande wake Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Sekondari ya Holili, Benson Samizi iliyopo eneo la Wilaya ya Rombo mpakani anabainisha kuwa mwitikio wa wazazi kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni hapo ni mdogo kabisa. Anasema hata wanapo itisha mkutano wa wazazi shuleni hapo mwitikio huwa ni mdogo pia, wazazi wengi huagiza wawakilishi baada ya kuja wao wenyewe.

“…Changamoto nyingine shuleni kwetu ni u-‘busy’ wa wazazi na biashara zao. Naamini wazazi wengi hapa hawafuatilii maendeleo ya watoto wao shuleni, mzazi utakuta unamuita kumshirikisha jambo kwa maendeleo ya manae lakini anatuma mwakilishi, majukumu yao kiusimamizi kwa mtoto anayatupa kwa mwalimu…sasa mwalimu hawezi kufanya kila kitu bila ushirikiano na mzazi,” anasema Samizi.

“Binafsi nilijaribu kufanya utafiti mdogo shuleni kwetu wa kuangalia ni kwa kiasi gani wazazi wanafuatilia maendeleo ya mtoto shuleni…lakini huwezi amini kwa mwaka mzima walikuja wazazi wawili tu wenyewe kuulizia maendeleo ya watoto wao, hapa unaweza kuangalia ni namna gani watu hawa wapo ‘busy’ na shughuli zao zaidi ya maendeleo ya mtoto shuleni. Hata ukiitisha kikao cha wazazi hawafiki robo tatu ya wanafunzi wanaokuja shuleni,” anasema mwalimu Samizi.

Aidha anakiri uwepo wa wanafunzi ambao hurubuniwa na kujiingiza katika shughuli nyingine nje ya masomo na wengine kuacha shule. Anasema kuwa kwa mwaka 2013 shule hiyo ilipewa jumla ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 140 lakini walioripoti ni wanafunzi 85 tu, huku wengine 30 kupelekwa katika shule za binafsi. idadi iliyosalia hawajulikani walipo hadi sasa. Anaongeza kuwa kuanzia mwaka 2011 hadi Mai 2013 jumla ya wanafunzi 7 walitiwa mimba na kesi zao kushughulikiwa katika hatua anuai.

Sim Msami Silayo ni Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Urauri iliyopo maeneo ya mpakani Wilaya ya Rombo, anasema tangu nyakati za ukoloni kulikuwa na kasumba ya wanafunzi kwenda kufanya vibarua maeneo ya mpakani anasema hali hii imeendelea mpaka leo. Anasema zipo baadhi ya familia zinautaratibu wa kwenda kufanya vibarua kwa makundi hivyo kuwaathiri baadhi ya wanafunzi.

Anasema kwa taarifa ambazo wanazo wapo baadhi ya mabinti hukimbia shule na kwenda kufanya kazi za uuzaji vinywaji baa na wengine kazi za majumbani hali ambayo uongozi wa shule umekuwa ukiendelea kupambana kukabiliana na changamoto hiyo.

Wakati hali iko hivyo wanafunzi kama Thabit Kayanda (si jina lake halisi) japokuwa ni mmoja wa wanafunzi wilayani Rombo wanamtazamo tofauti. “…Unapoona mzazi yupo ‘busy’ na biashara zake kiasi hata cha kutokutimizia mahitaji yako ya shule lazima uanze kujitengenezea maisha yako mwenyewe hivyo mtu unajikuta unaingia katika biashara au shughuli zingine kujipatia fedha. Na kama unafanya na kufanikiwa (kupata fedha) unajikuta unaona hakuna haja ya kuendelea na shule…kumbuka kila mmoja anasoma ili aje kupata fedha za kuendesha maisha yake, kama unaanza kufanikiwa chochote hakuna haja ya kuendelea na shule,” ni maneno ya Kayanda na mtazamo tofauti.  

Hata hivyo mtazamo wa wanafunzi kama Kayanda na changamoto nyingine zilizopo wilayani Rombo haziondoi umuhimu wa elimu kwa kila mtoto. Hivyo kila mmoja na kila upande unakila sababu ya kuhakikisha unatimiza wajibu wake na elimu kupewa kipaumbele maeneo yote bila kujali changamoto zilizopo.