Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura
TIMU ya Taifa ya wanawake ya mpira wa miguu (Twiga Stars) imepangwa kundi B
katika Michezo ya Afrika (All Africa Games). Michezo hiyo ya Kumi itafanyika
kuanzia Septemba 3-18 mwaka huu jijini Maputo, Msumbiji.
Upangaji makundi kwa ajili ya michezo hiyo kwa upande wa wanawake na wanaume
ulifanywa jana na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF),
Hicham El Amran.
Rais wa CAF, Issa Hayatou pia alishuhudia upangaji huo wa makundi uliofanyika
makao makuu ya shirikisho hilo jijini Cairo, Misri wakiwemo pia wawakilishi wa
timu zilizofuzu kwa ajili ya michezo hiyo.
Twiga Stars imepangwa pamoja na timu za Afrika Kusini, Zimbabwe na Ghana. Kundi
A lina wenyeji Msumbiji, Cameroon, Algeria na Guinea. Mabingwa wa mwaka 2007
Nigeria wameshindwa kufuzu kwa ajili ya michuano ya mwaka huu.
Wiki iliyopita Twiga Stars ilikuwa Harare, Zimbabwe kwenye mashindano ya Baraza
la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA). Ilishika nafasi ya tatu
ambapo ilicheza na Zimbabwe na Afrika Kusini. Zimbabwe ‘Mighty Warriors’ ndiyo
walioibuka mabingwa wakati Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’ ilikuwa makamu
bingwa.
Twiga Stars inayofundishwa na Charles Mkwasa akisaidiwa na Nasra Mohamed
inatarajia kuingia kambini mwezi mmoja kabla ya kuanza michuano hiyo
inayoshirikisha timu nane.
Kwa upande wa wanaume kundi A lina wenyeji Msumbiji, Afrika Kusini, Libya na
Madagascar wakati kundi B ni Cameroon, Uganda, Ghana na Senegal.
Boniface Wambura
Ofisa Habari