Twiga Stars Yajipanga Kupambana na Shepolopolo

Baadhi ya wachezaji wa Twiga Stars wakijinoa mazoezini

Baadhi ya wachezaji wa Twiga Stars wakijinoa mazoezini

TIMU ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) inaendelea kujinoa kwa ajili ya mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Zambia (Shepolopolo) itakayochezwa Februari 28 mwaka huu.

Twiga Stars chini ya Kocha Rogasian Kaijage na Msaidizi wake Nasra Juma inaendelea vizuri, na kwa mujibu wa programu ya benchi lao la ufundi kesho (Jumatatu), Jumanne na Jumatano itafanya mazoezi saa 10 jioni.

Mazoezi hayo yatafanyika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Uwanja huo ndiyo utakaotumika kwa ajili ya mechi hiyo itakayoanza saa 10 kamili jioni.

Shepolopolo ambayo ilishinda mechi ya kwanza mabao 2-1 wiki iliyopita inatarajiwa kuwasili nchini Alhamisi (Februari 27 mwaka huu) kwa ndege ya Fastjet, na siku hiyo hiyo itafanya mazoezi Azam Complex.

Waamuzi wa mechi hiyo Ines Niyonsaba, Jacqueline Ndimurukundo, Axelle Shikana na Suavis Iratunga, wote kutoka Burundi wanatarajiwa kuwasili nchini Jumatano.

YANGA, PRISONS KUPANGIWA TAREHE MPYA
Mechi namba 118 ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Tanzania Prisons iliyokuwa ichezwe Februari 26 mwaka huu itapangiwa tarehe nyingine. Uamuzi wa kuiondoa mechi hiyo iliyokuwa ichezwe Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam umefanywa ili kuipa fursa zaidi Yanga kujiandaa kwa mechi yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi Al Ahly ya Misri itakayofanyika Jumamosi (Machi 1 mwaka huu).

Al Ahly na Yanga zitarudiana wiki moja baadaye kati ya Machi 7, 8 au 9 mwaka huu jijini Cairo, Misri.

MECHI ZA MABORESHO TAIFA STARS
Mechi za mpango wa kuboresha Taifa Stars kati ya mikoa na mikoa wiki hii itakuwa kama ifuatavyo;

Februari 25 Njombe vs Ruvuma (Uwanja wa Njombe)

Kinondoni vs Ilala (Uwanja wa Karume)

Februari 26 Morogoro vs Pwani (Uwanja wa Jamhuri)

Geita vs Kagera (Uwanja wa Geita)

Kilimanjaro vs Tanga (Uwanja wa Ushirika)

Iringa vs Mbeya (Uwanja wa Samora)

Shinyanga vs Simiyu (Uwanja wa Kambarage)

Lindi vs Mtwara (Uwanja wa Ilulu)

Februari 27 Temeke vs Kinondoni (Uwanja wa Karume)