TWIGA STARS YAINGIA KAMBINI KUJIANDAA NA COSAFA

Baadhi ya wachezaji wa Twiga Stars wakishangilia moja ya magoli yao.

Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars) imeingia kambini Juni 24 mwaka huu kwenye hoteli ya Itumbi iliyoko Mwembechai, Dar es Salaam kujiandaa kwa michuano ya wanawake ya COSAFA itakayofanyika jijini Harare, Zimbabwe.

Twiga Stars inayofundishwa na Kocha Charles Boniface akisaidiwa na Nasra Mohamed imeingia kambini ikiwa na wachezaji 25 na inafanya mazoezi katika viwanja vya Tanganyika Packers ulioko Kawe na Karume.

Michuano hiyo ya Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA) inashirikisha timu nane na itaanza Julai 2 hadi 9 mwaka huu. Twiga Stars ambayo pia inajiwinda kwa michezo ya All Africa Games itakayofanyika Septemba mwaka huu jijini Maputo, Msumbiji inashiriki kama timu mwalikwa.

Timu nyingine zinazoshiriki michuano hiyo ambayo mechi zake zitachezwa katika viwanja vya Rufaro na Gwanzura ni Zimbabwe, Lesotho na Botswana. Nyingine ni Afrika Kusini, Zambia, Msumbiji na Malawi.

Twiga Stars ambayo imepangwa kundi A pamoja na wenyeji Zimbabwe, Lesotho na Botswana itacheza mechi yake ya kwanza Julai 2 mwaka huu dhidi ya Botswana kwenye Uwanja wa Gwanzura.

Siku inayofuata itacheza na Lesotho kwenye Uwanja wa Rufaro kabla ya kumaliza mechi za makundi Julai 5 mwaka huu kwa mechi dhidi ya wenyeji kwenye Uwanja wa Gwanzura.

Hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo itafanyika Julai 7 mwaka huu. Kila kundi linatoa timu mbili kuingia katika hatua hiyo na nusu fainali zote pamoja na fainali zitachezwa Uwanja wa Rufaro.

Boniface Wambura
Ofisa Habari