TWIGA STARS KUONDOKA JULAI MOSI KUSHIRIKI COSAFA

Baadhi ya wachezaji wa Twiga Stars

TIMU ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Wanawake (Twiga Stars) inatarajia kuondoka

Julai Mosi mwaka huu kwenda Harare, Zimbabwe kushiriki mashindano ya COSAFA

yanayoanza Julai 2 mwaka huu jijini humo.

Twiga Stars inayofundishwa na Kocha Charles Boniface akisaidiwa na Nasra Mohamed

itaondoka saa 11 alfajiri kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi ikiwa na

msafara wa watu 26.

Katika msafara huo wachezaji ni 19 huku benchi la ufundi likiwa watu wanne.

Kiongozi wa msafara ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake

Tanzania (TWFA) Lina Mhando ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Twiga Stars inashiriki michuano hiyo ya Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu

Kusini mwa Afrika (COSAFA) ikiwa timu mwalikwa. Jumla ya timu nane zinashiriki

wakiwemo wenyeji Zimbabwe.

Nyingine ni Lesotho, Botswana, Afrika Kusini, Zambia, Msumbiji na Malawi. Twiga

ambayo iko kundi A pamoja na Zimbabwe, Lesotho na Botswana itacheza mechi yake

ya kwanza Julai 2 mwaka huu dhidi ya Botswana kwenye Uwanja wa Gwanzura.

Siku inayofuata itacheza na Lesotho kwenye Uwanja wa Rufaro kabla ya kumaliza

mechi za makundi Julai 5 mwaka huu kwa mechi dhidi ya wenyeji kwenye Uwanja wa

Gwanzura.

Hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo itafanyika Julai 7 mwaka huu. Kila kundi

linatoa timu mbili kuingia katika hatua hiyo na nusu fainali zote pamoja na

fainali zitachezwa Uwanja wa Rufaro.

Boniface Wambura

Ofisa Habari