TWIGA STARS KUJIPIMA KWA BANYANA BANYANA

Timu ya taifa ya wanawake Twiga stars katika picha ya pamoja

Timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) inatarajia kucheza mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya Afrika Kusini (Banyana Banyana) itakayofanyika Mei 20 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Twiga Stars inayojiandaa kwa mechi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Ethiopia imeingia tena kambini jana (Mei 14 mwaka huu) kujiwinda kwa mechi hiyo itakayochezwa Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa.
Banyana Banyana pia iko katika kinyang’anyiro cha kutafuta tiketi ya Fainali za Nane za AWC ambapo katika raundi hii ya pili imepangiwa Zambia na itaanzia mechi hiyo ugenini jijini Lusaka.
Mei 12 mwaka huu Twiga Stars ilicheza mechi ya kimataifa ya kujipima nguvu dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors) iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kambi ya timu iko Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Ruvu mkoani Pwani.
Naye Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa katika kuimarisha kikosi chake kabla ya mechi ya Jumapili dhidi ya Banyana Banyana amemwita tena kikosi mshambuliaji mkongwe Esther Chabruma.
Wakati huo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Rwanda kuchezesha mechi hiyo ya AWC kati ya Tanzania (Twiga Stars) na Ethiopia.
Waamuzi hao ni Angelique Tuyishime atakayepuliza filimbi wakati waamuzi wasaidizi ni Sandrine Murangwa, Speciose Nyinawabari na Salma Mukansanga. Kamishna wa mchezo huo wa kwanza ni Catherine Adipo kutoka Uganda.
Mechi ya marudiano itachezwa Dar es Salaam wiki mbili baadaye ambapo mshindi atapata tiketi ya kucheza Fainali za Nane za AWC zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.