TWB-Benki inayohimiza matumizi ya ‘vibubu’

Mshauri wa Wateja kutoka Benki ya Wanawake Tanzania (TWB), Bi. Joan Mogori akionesha mfano wa kiboksi kidogo cha chuma (kibubu) ambacho ni moja ya huduma wanayoitoa kwa wateja wao katika Viwanja vya Mnazi Mmoja

Na Mwandishi Wetu

BENKI ya Wanawake Tanzania (TWB) ni miongoni mwa Taasisi za kifedha zinazoshiriki Maonesho ya Wajasiriamali Wanawake yanayoendele katika Viwanja vya Mnazi Mmoja. Inashiriki kwasababu ya kutangaza huduma zake mbalimbali inazozitoa kwa wateja wake na hasa wajasiriamali wanawake.

Lakini miongoni mwa huduma inazozitangaza ni ya matumizi ya ‘kibubu’ kuhifadhia fedha kwa muda kabla ya kuziwasilisha benki muda muafaka. Kwa wale wasiotambua nini maana ya kibubu, ni kwamba; kwa tafsiri sahisi isiyo rasmi- wapo baadhi ya watu hasa Watanzania wengu wa kipato cha chini awali walikuwa hawatumii benki kuhifadhi fedha zao.

Hawa walikuwa wakitumia kiboksi kidogo kilichotengenezwa kwa mbao na kuwekewa tundu dogo kwa ajili ya kuhifadhia fedha. Kiboksi hicho wengi wanakiita ‘kibubu’. Mtanzania wa aina hii aliweza kuweka fedha zake kidogo kidogo kwa muda fulani hadi zilipokuwa nyingi na baadaye hufungua na kuzifanyia alichokikusudia.

Bi. Joan M. wa Benki ya Wanawake Tanzania akionesha 'kibubu' alipozungumza na dev.kisakuzi.com, Tanzania


Njia ya kibubu bado inatumika hadi leo kwa baadhi ya Watanzania hasa wa kipato cha chini. TWB sasa wameamua kuenzi mfumo huo kwa kuweka maboresho zaidi. Wao wanampa Mtanzania kibubu chenye funguo na kisha kubaki na funguo za kibubu hicho kilichotengenezwa kwa chuma.

Yaani utaweza kukusanya fedha pasipo uwa na uwezo wa kuzitumia kabla ya ushauri wa benki yao. Huenda hii ikawa njia moja wapo ya kuwahimiza Watanzania kuona umuhimu wa matumizi ya benki.

Joan Mogori ni Mshauri wa Wateja wa Benki ya Wanawake (TWB), anasema wanaitumia njia hiyo kwa kumpa ushauri mteja wao au Mtanzania yeyote anayekubali kununua kiboksi hicho kwao.

Anasema si lazima mtu kuwa na akaunti katika benki hiyo, ndipo apewe huduma ya ‘kibubu’ la hasha. Anaweza kununua na kupewa huduma hiyo bila kuwa na akaunti yoyote kutoka TWB. Lakini ushauri tu kwa kila anapokuja kuangalia kiasi cha fedha alichohifadhi kwenye kiboksi hicho. Hata hivyo anasema wateja wao wanaweza kukitumia kiboksi hicho wakati wanapokuwa ama mbali na tawi la benki hiyo au kiasi kidogo cha kupeleka benki.

“Mfano mtu anakaa mbali na tawi la benki yetu hawezi kutoka huko na kuja kuleta sh. 10,000, lakini anaweza kuingiza kwenye kiboksi hiki na kuja baada ya muda fulani…atakapo kuja baada ya kipindi fulani tutafungua na kutoa kiasi anachotaka kisha kuingiza kwenye akaunti yake,” anasema Bi. Mogori alipokuwa akizungumza na dev.kisakuzi.com Viwanja vya Mnazi Mmoja.