Na Mwandishi Wetu
KATIKA kuhakikisha Watanzania wanakuwa na afya bora, kinywaji kisicho na kilevi cha Vita Malt, kimeandaa bonanza maalumu litakalowashirikisha wafanya mazoezi na litakalofanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa Vinywaji visivyo na Vileo katika Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Consolata Adam alisema, wameamua kuandaa bonanza hilo ili kuwakutanisha pamoja wafanya mazoezi wote, ambao mara nyingi wanafanyia katika vituo maalumu (gym).
Consolata alisema, bonanza hilo la aina yake kwa Dar es Salaam litafanyika katika Viwanja vya Posta vilivyopo Kijitonyama kuanzia saa 12 asubuhi ya Jumamosi.
“Tumeamua kuandaa bonanza linalowakutanisha wanamichezo mbalimbali hasa wafanya mazoezi ili kuweza kukutana na kufanya mazoezi kwa pamoja. Siku hiyo katika Viwanja vya Posta kutakuwa na gym kumi na mbili zilizo maarufu ambazo zitashiriki na kutakuwa na wakufunzi kumi ambao wataongozwa na mkufunzi wa kimataifa SAAS,” alisema, huku akidai mtu anatakiwa kwenda tu kwani mazoezi hayo yatakuwa bure.
Alisema, lengo kuu kuu la bonanza ni kuhamasisha jamii nzima kutambua umuhimu wa kufanya mazoezi ili kujenga afya bora za miili yao na pia kujenga umoja imara wa gym zilizopo nchini.
Consolata alisema, katika kuhakikisha bonanza hilo linakuwa bora na la kufana jumla ya gym kumi na mbili zitashiriki ambazo ni Better Life, Genessis ya Kijitonyama, Segerea Gym, Rio Gym, Genessis ya Kimara, Azula ya Mikocheni na Serena Gym.
Alisema pia baa zilizoshinda katika kuchoma nyama katika mashindano yaliyofanyika hivi karibuni za Fyatanga ya Tegeta na Kisuma Bar ya Temeke, zitaonyeshana umwamba kwa kuchoma nyama bomba kwa kipindi chote hicho.
“Tumeweka burudani za kila aina kwani kutakuwa na michezo mbalimbali ya kufurahisha kama soka, netiboli, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, Sehemu za watoto kuchezea pia na zawadi nyingi toka Vita Malt zitakuwepo.”
NaYe Meneja Mawasiliano na Mahusiano wa TBL, Edith Mushi alisema mbali na hayo kutakuwa na burudani mbalimbali toka kwa bendi African Stars ‘Twanga Pepeta’ na msanii mkali wa Hip hop, Roma Mkatoliki sambamba na burudani nyingine nyingi kwa kipindi chote cha tamasha.
“Hii ni siku ya familia napenda kuwajulisha watanzania wote na wapenda michezo kote nchini kuwa waje mapema na familia zao siku ya Jumamosi, hakutakuwa na kiingilio chochote na vinywaji vyote toka TBL vitakuwepo.
“Lakini pia watu wa kawaida na wa rika zote siku hiyo hakutakuwa na kikwazo chochote cha kufanya mazoezi, kwani ni bure kabisa, hivyo nawashauri tufike kwa pamoja ili tuweze kupata pia ushauri mbalimbali juu ya kupunguza uzito na aina ya mazoezi yanayotakiwa,” alisema.
Vita Malt ni kinyaji kinachozalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).