‘Tutaendelea kulinda uhuru wa kuabudu dini zote Zanzibar’

”]
”]

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema itaendelea kulinda uhuru wa dini zote ikiwa ni pamoja na kutokubali kuvumilia vitendo vyovyote vya uvunjaji wa sheria vinavyofanywa na baadhi ya watu kwa mwamvuli wa kidini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, ameyasema hayo Aprili 15 katika hotuba yake aliyoitoa kwenye hafla ya kumuweka Wakfu kwa Askofu wa 10 wa Dayosisi ya Zanzibar, Askofu Michael Henry Hafidh.

Alisema kuwa ustawi wa dini mbalimbali Zanzibar unahusika na Sera ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya uhuru wa kuachia makanisa kuendesha seminari zao na makongamano bila ya kuingiliwa, huku akisisitiza uadilifu kwa viongozi wa dini.

Alieleza kuwa kwa kiasi kikubwa shughuli hizi za kidini zimekuwa zikiendeshwa kwa amani ambapo kwa bahati mbaya pamoja na hayo kumekuwepo nyakati ambapo kutofahamiana kumejitokeza katika baadhi ya makongamano.

“Serikali imeweka utaratibu maalum wa utoaji ruhusa wa makongamano hayo, taratibu hizo ni pamoja na utunzaji wa amani na kutobughudhiana kidini… tuelewe sote kwamba viongozi wa dini ni walimu na walezi wa jamii na wanadhamana kubwa mbele ya MwenyeziMungu”,alisema Dk. Shein.
”]
Aidha, alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kufanya kila linalowezekana kulinda haki za Watanzania katika kufuata dini na kuabudu dini waitakayo na kuishi bila ya kubaguliwa kutokana na sababu ya dini, kabila au rangi.

Alisema kuwa hakuna budi wananchi wote kwa pamoja kujivunia na kuiendeleza hali ya amani na utulivu iliyopo hapa nchini ambapo ziko nchi mbali mbali wamekuwa wakikosa hali hiyo kwa sababu ya migogoro inayotokana na sababu mbali mbali zikiwemo za kidini, kisiasa na kikabila,

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa licha ya kuwa Tanzania haina dini ya serikali kama ilivyokuwa ikisisitizwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na viongozi wa amamu zilizofuata lakini Watanzania walio wengi ni wafuasi na waumini wa dini zenye madhehebu tofauti.

Kutokana na hilo Dk. Shein alisisitiza kuwa jukumu la kulinda heshima baina wananchi na usalamaw a nchi linategemea sana mafunzo yanayofundishwa na yanayohutubiwa na viongozi katika nyumba za ibada.

Pia, alisisitiza viongozi wa dini mbali mbali wana wajibu wa kuhakikisha sehemu za ibada zinatumika kwa ibada tu bila ya kuingiza mambo mengine na kutoa wito kwa Jumuiya zote za kidini na wananchi kuendelea kuheshimiana na kuishi bila ya kubaguana.

“Sote tuwe na lengo moja la kuiletea maendeleo nchi yetu kwa manufaa ya watu wake wote’, alisema Dk. Shein. Pia Dk. Shein aliwaeleza waumini hao kuwa mambo yao waliyomueleza ameyasikia na atayafanyia kazi.

Alisema kuwa anafarajika kuona kuwa taasisi mbali mbali za kidini zinaendeleza juhudi zao za kutoa michango katika sekta mbali mbali za maendeleo na za kijamii ambapo pia alitumia fursa hiyo kulisisitiza kanisa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbali mbali zinazoikabili jamii. Sambamba na hayo Dk. Shein alisema kuwa jambo linalokubaliwa na ulimwengu wote ni kwamba Zanzibar ina watu wa dini mbali mbali ambao wanaendesha shughuli na ibada zao katika mazingira huru bila ya wafuasi wao kubughudhiawa.

Alisema kuwa historia hiyo ya uvumilivu wa dini Zanzibar ni ndefu na zikiangaliwa kumbukumbu itaonekana kwamba Wamishonari wa dini mbali mbali wamepokelewa na kuepwa fursa kadhaa nchini ambapo miongoi mw hao ni Dk. Livingstone ambaye alifanya ziara Zanzibar baina ya miaka 1983 na 1856.

Mapema Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Mhashamu Dk. Valentino Mokiwa, alieleza kuwa leo Dayosisi hiyo imepata Askofu baada ya muda mrefu tangu kifo cha Askofu Mhashamu Douglas Toto. Aliwasisitiza waumini wa kanisa hilo kumpa heshima na msaada mkubwa Askofu wao huyo mpya na bila ya kumbeza, kumdharau na badala yake wampe ushirikiano mkubwa.

Naye Askofu Michael Henry Hafidh, alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kuwaunga mkono waumini hao katika siku yao hiyo ya kihistoria. Pamoja na hayo, Askofu huyo alieleza kuwa kanisa kama taaisisi ya kijamii inao wajibu wa kuhakikisha kuwa mahusiano mema na serikali yanadumishwa. Aidha serikali kwa upande wake inao wajibu wa kuhakikisha kuwa inatoa haki stahiki kwa raia wake bila bila ya kujali itikadi zao z kidini, kisiasa, maeneo wanayotoka, wingi ama uchache wao katika nchi.

Askofu huyo katika hotuba yake pia aliomba kutafutiwa ufumbuzi changamoto kadhaa zinazowakabili waumini hao ikiwemo masuala ya ardhi na mengineyo. Pamoja na hayo, Askofu huyo alimueleza Dk. Shein kuwa anafahamu kuwa kutajitokeza watu wachache ambao watahoji ushiriki wake katika hafla hiyo na kueleza kuwa yeye amekwenda pale si kwa ajili ya kuabudu bali kuwaangalia wananchi wake ambao wamo waliomchagua.

Aidha, alieleza kuwa elimu itaendelea kupewa msukumo zaidi kwa kuimarisha mfumo wa elimu wa Dayosisi ili vijana wengi zaidi wapate fursa ya elimu ya juu kwa mustakbali wa Kanisa na nchi yao sanjari na kuendeleza Mkakati wa Kupunguza Umasikini MKUZA.

Maaskofu mbali mbali walihudhuria pamoja na waumini wengine na viongozi kadhaa akiwemo Raia mstaafu Benjamin Mkapa, Waziri Mkuu Mstaafu na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Joseph Warioba, Jaji Agostino Ramadhani, Waziri Mkuchika, baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na viongozi wengine. Kuwekwa Wakfu Askofu huyo wa Zanzibar kulitanguliwa na ibada ya ushirika Mtakatifu ambayo iliongozwa na Askofu Mkuu Dk. Valentino Mokiwa.