Na Joachim Mushi, Dar es Salaam
MGOMBEA mwenza wa nafasi ya urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Samia Suluhu amesema Serikali watakayoiunda endapo watapewa ridhaa ya kuongoza nchi watahakikisha wanadhibiti wizi wa dawa kwenye hospitali za Serikali ambazo zimekuwa zikiuziwa wananchi katika maduka ya dawa mitaani.
Bi. Suluhu katoa kauli hiyo jana alipokuwa akihutubia katika mikutano ya anuai ya hadhara Jimbo la Ilala kuinadi ilani ya Chama Cha Mapinduzi, ambapo amebainisha kuwa dawa zote zitakuwa zinaingizwa katika mtandao maalum na kuzifuatilia na endapo zitatumika nje ya utaratibu itabainika na hatua kuchukuliwa.
Alisema mtandao huo utafanikiwa kukabiliana na kero ya ukosefu wa dawa katika hospitali za serikali kwani dawa hizo zimekuwa zikiibwa kwenye hospitali za Serikali na kuuzwa nje katika maduka ya dawa binafsi na hospitali binafsi. “…Tunaamini mfumo huu utatusaidia kukabiliana na wizi wa dawa na rushwa hospitalini…unakuta daktari anakuandikia dawa alafu anakuelekeza duka la kwenda kununua sasa unajiuliza huyu mtu kajuaje kama sio yeye kapeleka pale,” alisema Bi. Suluhu.
Pamoja na hayo mgombea huyo mwenza, aliwashauri wananchi kuukubali utaratibu wa kutumia mfumo wa bima ya afya kwa matibabu ambao umekuwa ukimlazimu mwananchi kuchangia kiasi kidogo cha fedha na kutibiwa mwaka mzima bure katika hospitali zote zinazotumia utaratibu huo, kwani alidai utawasaidia wengi. “…Unajua ugonjwa unampata mtu ghafla na muda wowote haijalishi una fedha za kujitibu au la, lakini kama unabima ya afya waweza kutibiwa muda wowote hata kama hauna fedha wakati huo,” alisisitiza Bi. Suluhu.
Aidha, Bi. Suluhu alisema serikali watakayoiunda itajitahidi kupima maeneo mengi ya ardhi na kuyatoa kwa wananchi ili kukabiliana na migogoro ya ardhi. Alisema Serikali yao pia imekamilisha utaratibu wa kuwalipa fidia wananchi wa Kipunguni ambao wanadai fidia na itawalipa wananchi hao kwa thamani ya sasa ya ardhi kwani 2004 hadi sasa ni muda mrefu na ardhi imepanda thamani.
Akizungumzia kero ya foleni, alisema ili kumaliza kero hiyo na msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, Serikali imepanga kujenga miji mipya maalum na ya kisasa pembezoni wa jiji hili na kwa kuanzia itajenga mjini huo eneo la Kibaha ili shughuli nyingine ziwe zikifanyika katika mji huo na Dar es Salaam kupunguza msongamano, zoezi litakaloenda sambamba na ujenzi wa barabara ndogondogo za mitaani ambao utapunguza msongamano na foleni katika barabara kubwa.
Aidha Bi. Suluhu alisema zitajengwa barabara za juu katika makutano ya barabara ikiwa pamoja na kuzijenga barabara ndogondogo zikiwemo za Mbezi Morogoro-Malamba Mawili-Tangi Bovu-Kimara Baruti-Goba na nyinginezo ili kupunguza msongamano katika barabara kubwa.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com