Na Edwin Moshi, Kilimanjaro
IMEELEZWA kuwa kujituma, kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano mzuri na viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya chini ni moja ya mafanikio yanaolifanya shirika la TUSONGE kukubalika kwa wananchi wanaofanya nao kazi.
Hayo yamesemwa na mkurugenzi wa shirika la TUSONGE lililopo Moshi mkoani Kilimanjaro Bi. Aginatha Rutazaa (aliyesimama pichani) wakati akizungumza na wafanyakazi wa shirika la SUMASESU lililopo wilayani Makete mkoani Njombe lilipofanya ziara katika shirika hilo yenye lengo la kubadilishana mawazo na kujifunza mbinu mbalimbali wanazozitumia kufikisha ujumbe kwa jamii.
Bi Aginatha amesema wakati wa ufanyajikazi katika shirika lake wamekuwa wakishirikiana kwa pamoja na wananchi pamoja na viongozi wa serikali ikiwemo mitaa na vijiji ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo wenye watu na ukiwashirikisha ni rahisi ujumbe kufika kwa jamii.
Shirika hilo ambalo linatoa elimu ya mambo mbalimbali kwa wananchi ikiwemo UKIMWI na ujasiriamali, limefanikiwa kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa kwa wajasiriamali wadogo (wa hali ya chini) ambapo walipata wasaa wa kutembelea kikundi kimojawapo kilichopo kata ya Karanga na kujionea kinavyofanya kazi.
Pia amesema wanatumia video kuonesha elimu mbalimbali hasa magonjwa ya ngono na UKIMWI ili ujumbe ufike moja kwa moja kwa jamii na kuona hali halisi ya kile kinachozungumziwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa SUMASESU, Egnatio Mtawa alishukuru kwa mapokezi mazuri ya shirika la TUSONGE ambapo pamoja na mambo mengine alikiri kujifunza mengi mazuri kutoka kwao na kuahidi kwenda kuyatumia kwenye shirika lake ili jamii iweze kusonga mbele.