‘Tusiidharau Elimu ya Watu Wazima…!’

Elimu ya watu wazima

Elimu ya watu wazima

Yohane Gervas, Rombo

WANANCHI wilayani Rombo wameshauriwa kuondokana na dhana potofu ya kupuuzia na kuidharau elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi kwani elimu hiyo inawasaidia kubadili mtazamo na kukabiliana na changamoto za maisha.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wa wilaya ya Rombo, Emanueli Buruge ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Rombo katika kilele cha maadhimisho ya juma la elimu ya watu wazima yaliyofanyika katika ukumbi wa chuo cha maendeleo ya wananchi mamtukuna.

Amesema kuwa wananchi wengi wanashindwa kukabiliana na changamoto za maisha kutokana na kukosa elimu hivyo wanabakia katika wimbi la umasikini, aidha amewataka viongozi wanaohusika kuwahimiza wananchi kujiunga na elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi kwani bado ina umuhimu
mkubwa kwao.

Awali Ofisa elimu ya watu wazima, Efremu Shayo, akimkaribisha mgeni rasmi amesema kuwa wananchi wengi wanadhani kuwa elimu ya watu wazima imepitwa na wakati jambo ambalo si kweli. Pia amesema kuwa elimu ya watu wazima sio kufundisha kusoma na kuandika tu bali wanafundishwa ujuzi mbalimbali wa namna ya kupambana na umasikini katika jamii zao.