Na Eleuteri Mangi – MAELEZO
WALEZI wametakiwa kuwaelimisha, kuwalinda, kuwaandaa na kuwajali watoto wa kike namna ya kupambana na changamoto mbalimbali za kijinsia zinazowakumba watoto hao wakati wakiwe shuleni na hata nyumbani wa likizo. Kauli hiyo imetolewa na Mwezeshaji kutoka TUSEME wa masuala ya Ufundishaji ambao ni Rafiki Kijinsia Anita Masaki wakati wa semina ya siku tano kwa walimu na watumishi wasio waalimu wa Shule ya Wasichana ya WAMA-Nakayama iliyopo kijiji cha Nyamisati walayani Rufiji mkoa wa Pwani.
Anita amewataka walezi hao kutambaua dhamana waliyopewa na wazazi wa watoto hao na taifa kwa ujumla ya kuwaandaa vema wanafunzi hao kitaaluma na watambue umuhimu wao wenyewe na kwa taifa. Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa mtoto wa kike wa taasisi ya WAMA Mikidadi Alawi akimkaribisha Mwezeshaji wa semina hiyo alitoa taarifa fupi ya shule hiyo kuwa ina idadi ya wanafunzi 400 tangu kuanzishwa kwake ambapo kwa sasa wapo wanafunzi 363.
Alawi alisema kuwa shule ya WAMA-Nakayama ilianzishwa kwa lengo la kuwalea watoto wa kike wanaoishi katika mazingira magumu ambapo wanatoka mikoa yote nchini. Naye Mlezi wa Wanafunzi shuleni hapo Sarah Ngonde amesema kuwa wamenufaika na semina hiyo kwa kuwa imekuja wakati mwafaka kuimarisha maarifa yao ya namna ya kuwalea wanafunzi hao ili kuwasaidia wafikie malengo yao na hatimaye kuwa raia wema nchini.
Sarah alisema kuwa wanaamini watakapo maliza semina hiyo watakuwa wanajua zaidi namna ya kuangalia masuala ya kijinjsia katika shuleni hapo na hata watakapokuwa na familia zao nyumbani. Shule ya Wasichana ya WAMA- Nakayama inayomilikiwa na taasisi isiyo ya serikali ya WAMA inatoa elimu ya sekondari kwa wasichana kidato cha kwanza hadi sita ilizinduliwa rasmi Septemba 24, 2011 na Rais wa Serlikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwnyekiti wa Baraza la Mapinduzi Ali Mohamed Shein.