TUNYWE VIKOMBE BILA KUPOTEZA MWELEKEO!

    

 Ni siku chache tu zimepita toka nimsikie Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Ndugu James Mbatia akielezea hofu na masikitiko yake juu ya hili suala ninaloita kupoteza muelekeo! Mbatia alikuwa analizungumzia suala la Loliondo kwa ‘Babu’ lilivyoshika kasi mpaka kutishia utowekaji wa hoja nyingine za msingi kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu.

Nasema hoja ‘nyingine za msingi’ kwasababu si kwamba napinga ati lile la Loliondo si la msingi. Suala la dawa ya babu ni la msingi na matumaini yangu ni kwamba yote mazuri ninayosikia kuhusu huko Loliondo yawe ni kweli, kwasababu taifa lenye afya ni bora kuliko taifa gonjwa! Kama ni ukweli au uwongo, hilo ni suala la nyakati kutudhihirishia. 

Nafikiri sio ‘realistic’ kuwaambia watu wasiende Loliondo kutafuta dawa ya maradhi yanayowasumbua. Ni suala la uwamuzi binafsi, kwa wale walioamua kuelekea Loliondo na wale wengine walioamua kusubiri mpaka hapo watakapo thibitisha kile wanachokisikia. Kama wewe au mimi sio wagonjwa au hatuna ndugu wala jamaa anayeugua, si rahisi kuelewa kwanini watu wamefurika Loliondo. Kwahiyo, la hasha siwezi kusema linaloendelea Loliondo nyumbani kwa Mchungaji mstaafu Ambilikile Mwasapile si la msingi. Isipokuwa, kama Mbatia na wengine walivyosema ni hatari kwa taifa kama gumzo zima nchini litakuwa ni Loliondo!

Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumepoteza muelekeo wa hoja nyingine za msingi, ambazo ni Katiba mpya, Umeme wa uhakika, Hospitali bora na vita dhidi ya ufisadi. Hayo ndio haswa matatizo ya taifa letu kwasasa na kwa bahati nzuri au mbaya hatotokea ‘nabii’ wa kututibu kama Ambilikile Mwasapile. ‘Manabii’ wa matatizo haya ni Watanzania wote, hivyo basi itakuwa ni kosa la ‘jinai’ kuacha kuendeleza msisitizo wa matatizo ya taifa na badala yake kuanza kujadili Loliondo kuanzia asubuhi mpaka usiku.

Baadhi ya viongozi wetu serikalini wamekuwa wanalisemea suala hili la Loliondo kwa nguvu sana (Mpaka najiuliza hivi wangekuwa wepesi kuzungumzia masuala mengine nyeti namna hii, si tungekuwa mbali sana?) Tayari kumeshakuwa na hoja kwamba serikali inatumia mwanya huu kupoteza muelekeo wa masuala nyeti. Kama Watanzania, inabidi tuwe wabishi kama hicho kikaragosi hapo juu na tuendelee kuuliza  maswali nyeti bila kuchoka. Huu si wakati wa kuwaachia viongozi wetu kutuchagulia ngoma gani ya kucheza, kwani tukiwa kama wachezaji tunao uhuru wa kuchagua ni ngoma gani tunataka kucheza.

Bunge letu tukufu litarudi kazini Aprili 5 mwaka huu, ni matumaini yangu kwamba hoja za Katiba mpya, Umeme wa uhakika, Hospitali bora na vita dhidi ya ufisadi zitatawala bunge zaidi. Mpaka hapa tulipofikia, suala la Loliondo tuwaachie Wizara ya Afya na taasisi nyingine husika waendelee kulishughulikia. WE GOT A JOB TO DO!!

By Rungwe Jr.

rungwe@dev.kisakuzi.com