TUNDU LISSU MATATANI

Mbunge wa Singida Mashariki, Mh. Tundu Lissu

 

 

SPIKA Anne Makinda, amempa siku mbili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kuthibitisha kauli yake aliyoitoa bungeni jana kwamba Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja ni mwongo.

Alisema mbali na Lissu kuthibitisha kauli yake, yeye (Spika) atatoa taarifa juu ya Mbunge wa Arusha, Godbless Lema (Chadema), ambaye kwenye Mkutano uliopita alitaka kujua hatua zinazochukuliwa kwa kiongozi kama Waziri Mkuu anapolidanganya Bunge.

Makinda alitoa uamuzi dhidi ya Lissu bungeni jana baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.

Alisema kutokana na kauli ya Lissu ya kumuita Waziri Ngeleja kuwa ni mwongo, atatakiwa kuuthibitisha uongo wake keshokutwa.

“Tundu Lissu atatakiwa kuandika maelezo yake na kuyawasilisha kwangu siku ya Ijumaa ili yaweze kufanyiwa kazi… maelezo hayo yatafanyiwa kazi na vyombo vyangu pamoja na Kamati ya Maadili, baadaye Lissu na Waziri Ngeleja wataitwa ili kila mmoja kubainisha ukweli wake,” alisema.

Alisema baada ya ukweli kubainika, ataitoa taarifa hiyo bungeni. Awali, katika tukio hilo katika kipindi cha maswali na majibu, Lissu aliomba mwongozo wa Spika baada ya Waziri Ngeleja kujibu swali lake la nyongeza.

“Mheshimiwa Spika naomba mwongozo wa Spika kwa mujibu wa kanuni ya 63 (i) na 64 (a) kuhusu kutokusema uongo bungeni, Waziri amesema uongo bungeni,” alisema.

Kutokana na mwongozo huo, Spika aliahidi kumpa nafasi mbunge huyo athibitishe uongo wa Ngeleja.

“Hapa ndani ya Bunge hatuwezi kujua nani anasema uongo ila tutakupa nafasi ututhibitishie, utuletee,” alisema Makinda.

Katika swali la nyongeza Lissu alitaka kujua ni kwa nini mwekezaji aliyepewa leseni ya kutafuta madini ya dhahabu katika Wilaya ya Singida, kampuni ya Shanta Mining, anajenga kiwanja cha ndege katika maeneo ya makazi bila kulipa fidia.

Kwa mujibu wa Lissu, mwekezaji huyo pia ametwaa kwa nguvu maeneo ya vijiji viwili vya wilaya hiyo bila kufuata sheria.

Akijibu swali hilo, Ngeleja alisema ujenzi wa kiwanja hicho pamoja na meneo yaliyochukuliwa na mwekezaji huyo yapo kisheria na kuwa mwekezaji huyo hajaenda kinyume cha sheria.

Alisema si kweli kama eneo lililojengwa kiwanja cha ndege limechukuliwa kinyume cha sheria, bali taratibu zote zimefuatwa na zinaendelea kufuatwa.

Source: Mtanzania