LEO siku nzima kamati ya PAC ilikuwa inazungumza na Bodi ya Sukari, Wizara ya Kilimo na Wakulima wa Miwa Wilayani Kilombero. Tanzania huzalisha wastani wa tani 300,000 za Sukari kwa mwaka ilhali mahitaji ni tani 420,000 kwa mwaka. Hii hupelekea uagizaji wa Sukari kutoka nje ambao umekumbwa na malalamiko makubwa sana kutoka kwa wadau mbalimbali.
Masuala kadhaa yameibuliwa katika kikao cha leo
Wakulima wamelalamikia sana uingizaji holela wa Sukari nchini. Bei ya Miwa imeshuka kutoka tshs 69,000 kwa tani mpaka tshs 55,000 sababu ya Sukari ya ndani kukosa soko. Wakulima wamelalamikia viwanda kwa kujipangia bei bila kuwashirikisha wao na pia viwanda ndio vinapima Miwa na ubora wa mua wa mkulima hivyo kuleta mgongano mkubwa wa MASLAHI kwa mwekezaji.
Wakulima wametaka hisa 25% za Serikali katika viwanda vya Sukari wapewe wao ili waweze kushiriki katika Uchumi wa nchi. Bodi ya Sukari imeshindwa kuendeleza mradi wa RUIPA kwa sababu ya kutokuwa na Fedha tshs 11 bilioni za kulipa fidia ya Wananchi katika eneo la mradi. Mradi huu ungeweza kuzalisha tani 244,000 za Sukari kwa mwaka.
Wakulima wamelalamikia sana tabia ya viwanda kushindwa kununua Miwa yote ya Wakulima na hivyo kupelekea takribani nusu tu ya Miwa kutumika na nusu nyingine kubaki mashambani na kuharibika. Wastani wa tani 400,000 za Miwa huharibika Wilayani Kilombero peke yake. Hii ni sawa na tani 50,000 za Sukari.
PAC imetoa ufafanuzi wa masuala yafuatayo
Kamati ilikwishaiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania kufanya uchunguzi wa kikodi katika Sekta nzima ya Sukari nchini. TRA wameijulisha kamati kwamba wanafanyia kazi suala hilo na wameomba muda zaidi ili kukamilisha kazi hiyo. PAC imekubaliana na ombi hilo na pia kwamba inasubiri Taarifa ya kikosi kazi kilichoundwa na Katibu Mkuu Kiongozi ili kupata suluhisho la kudumu la Changamoto zinazokabili Sekta ya Sukari. Kamati ikishapata taarifa zote hizo itazifanyia kazi na kuziwasilisha Bungeni.
Kamati imeielekeza Bodi ya Sukari kuhakikisha inaendeleza mradi wa RUIPA kwa kutangaza zabuni ya kumpata mwekezaji ambaye atalima sehemu ya shamba na kumilikisha kwa hati Wakulima (outgrowers) sehemu nyingine ya shamba. Mradi wa RUIPA uwe mfano wa ushiriki wa wananchi katika Kilimo cha kisasa. Wakulima wamilikishwe Ardhi ya kulima Miwa na kuuza kwenye kiwanda, wasikodishiwe Ardhi hiyo. Bodi ya Sukari ipate FEDHA tshs 11 bilioni za fidia ya wananchi kutokana na zabuni ya kupata mwekezaji na malipo tangulizi ya mwekezaji.
Modeli ya Malaysia yaweza kutumika katika mradi wa RUIPA, kwa kuwagawia wananchi (households) 1500 wanaoathiriwa na mradi kila mmoja hekta 5 (4 za kulima Miwa na 1 ya makazi yake) na hekta zinazobakia katika jumla ya hekta 14700 ziwe nucleus. Ushiriki wa wananchi katika uzalishaji wa Ndio njia endelevu ya kutokomeza umasikini nchini.
Kamati imeelekeza kuwa Bodi ya Sukari iwe na mamlaka ya kuwa mdhibiti (regulator) kwa kutoa bei elekezi za mauzo ya Miwa na Sukari nchini ili kulinda Wakulima dhidi ya unyonyaji wa wawekezaji. Bodi pia ihusike na udhibiti katika upimaji wa Miwa na kiwango cha Sukari katika Miwa (sucrose) ili kujibu Changamoto ya Wakulima kupunjwa.
Kamati imeelekeza kuwa vianzishwe viwanda vya ngazi ya kati vya Sukari ili kutumia Miwa ya ziada na kuzalisha Sukari na hivyo kuongeza uzalishaji. Vyama vya Wakulima wa Sukari vimehamasishwa kuanzisha viwanda vidogo hivyo na Bodi ya Sukari imeelekezwa kulegeza masharti ya uanzishaji wa viwanda vya ngazi ya kati.
PAC imepingana na Wakulima kwamba hisa za Kampuni 25% wapewe wao na badala yake PAC imeelekeza Msajili wa Hazina aangalie uwezekano wa kuorodhesha hisa za Serikali katika soko la hisa la Dar Es Salaam na vyama vya Wakulima vipewe fursa kununua sehemu ya hisa hizo (angalau 5%).
Wakulima wa Miwa wamehamasishwa kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili wafaidike na mafao ya muda mrefu na muda mfupi ikiwemo Bima ya Afya, mikopo katika SACCOS zao na pensheni uzeeni. Tanzania ina jumla ya Wakulima wa Miwa (out-growers) 19,000 wenye kuzalisha nusu ya Sukari inayozalishwa nchini.
Tukipunguza upotevu wa Miwa ya Sukari (wastage) nchi nzima kwa kuanzisha viwanda vya Kati vya kusindika Miwa, tunaweza kuongeza uzalishaji kwa zaidi ya tani 80,000 za Sukari na kupunguza Sukari inayoagizwa kutoka nje. Tukitekeleza mradi wa RUIPA, tutakuwa na Sukari ya ziada tani 200,000 ambazo tunaweza kuuza nje na kupata fedha za kigeni. Hii iwe mikakati ya muda mfupi. Tunaweza tukiamua na kashfa za Sukari zitakuwa Historia. Tufanye sasa.
Imeandaliwa na Zitto Kabwe (MB)