Tunaumaliza Mwaka 2013 Nchi Ikiwa Salama; JK

RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete

RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete

RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewapongeza wa Tanzania kwa ujumla pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuhakikisha nchi imemaliza mwaka 2013 ikiwa na usalama. Rais Kikwete ametoa pongezi hizo leo katika hotuba yake ya kila mwezi kuzungumza na Watanzania.

“…Tunaumaliza mwaka 2013 nchi yetu ikiwa salama na tulivu. Mipaka iko salama na ile hali ya wasiwasi tuliyokuwa nayo kwa nyakati fulani mwaka huu sasa haipo tena. Uhusiano wetu na majirani ni mzuri na tutaendelea kufanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa hali inaendelea kuwa hivyo au hata kuwa bora zaidi mwaka 2014 na daima dumu.
Hali ya usalama wa ndani ya nchi nayo ni nzuri,” alisema Rais Kikwete.

Alisema hali ya wasiwasi iliyokuwa nayo Tanzania mwaka wa jana na mwanzoni mwa mwaka huu kuhusu uhusiano baina ya Wakristo na Waislamu haipo tena, na anaamini hali hiyo ya wasiwasi haitajirudia tena. “…Pepo mbaya amepita tuombe atokomee kabisa.”

Aliwataka Watanzania kuendelea kuishi pamoja kwa upendo, umoja, kuvumiliana na kushirikiana, ikiwa ni pamoja na kuepuka kugeuza tofauti za kisiasa, kidini, rangi, kabila au maeneo tutokayo kuwa chanzo cha uadui na mifarakano.

“…Kwa sasa tuna mwelekeo mzuri nawaomba tuudumishe. Mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni mwananchi. Tuchague kuijenga nchi yetu badala ya kuibomoa. Tusiwasikilize watu hasidi wanaochochea uadui na mifarakano miongoni mwetu. Watatuvurugia nchi yetu nzuri,” alisema Rais Katika hotuba yake.

Alisema katika mwaka 2013 kuna mafanikio ya vyombo vya dola kwa kushirikiana na wananchi kupambana na vitendo vya uhalifu, kwani hadi sasa mafanikio yaliyopatikana yanatia moyo licha ya hali hiyo kuendelea kuimarika. Alisema takwimu zinaonesha kwa Mwaka 2012 matukio ya ujambazi yaliyoripotiwa yalikuwa 6,872 huku kwa mwaka 2013 yakipungua hadi kufikia matukio 6,409.

“…Kati ya Januari na Desemba 2013, kilo 1,261 za heroin, kilo 3 za cocaine na kilo 89,293 za bangi zimekamatwa na watuhumiwa 1,631 wametiwa mbaroni. Tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa na mapambano yanazidi kuwa makali. Mafanikio yanaendelea kupatikana ingawaje bado tuna kazi kubwa na ngumu ya kufanya mbele yetu. Ni makusudio yetu kuongeza maradufu nguvu ya kupambana dhidi ya uhalifu huu.”

“Tupo hatua nzuri katika matayarisho ya kuanzisha Kikosi Maalum cha Kupambana na Dawa za Kulevya katika mwaka wa fedha 2014/15. Pia tutaitazama upya sheria ya adhabu kwa makosa ya kufanya biashara ya dawa za kulevya ili kuifanya iwe na meno makali zaidi. Vilevile, tutaongeza uwekezaji katika vituo vya tiba na kuwarekebisha watu wanaotumia dawa za kulevya. Mafanikio yanayopatikana Muhimbili na Mwananyamala yanatupa moyo wa kufanya zaidi,” alisema Kikwete.

Alisema Jeshi la Polisi limeendelea kupambana na ujambazi wa kutumia silaha na mafanikio yameendelea kupatikana, kwani matukio ya ujambazi yemepungua mwaka 2013 ukilinganisha na mwaka 2012; takwimu zinaonesha mwaka 2012 matukio ya ujambazi yaliyoripotiwa yalikuwa 6,872 na kwa mwaka 2013 yameripotiwa matukio 6,409.

“…Mwezi Julai mwaka huu, niliamua kulihusisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania katika kupambana na ujambazi wa kutumia silaha na utekaji wa magari katika Mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma. Katika Mikoa hiyo tatizo la ujambazi lilikuwa limefikia kiasi cha kulazimisha watu kusindikizwa na Polisi kutoka Ngara kwenda Karagwe, Biharamulo kwenda Muleba na kutoka Nyakanazi hadi Kakonko. Hali hii haikubaliki na hatuwezi kuiacha iendelee.” aliongeza JK.

“…Tumefika mahala pazuri katika mchakato wetu wa kutayarisha Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jana Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba, alitukabidhi Rasimu ya Pili ya Katiba, mimi na Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein. Kama nilivyosema jana kinachofuata sasa ni kuitangaza Rasimu hiyo katika Gazeti la Serikali kwa kila mtu na hasa Wajumbe wa Bunge la Katiba, kuiona na kuisoma. Baada ya hapo kitafuata kitendo cha kuifikisha Rasimu kwenye Bunge Maalum la Katiba kwa ajili ya kujadiliwa na hatimaye kupatikana Rasimu ya Mwisho itakayofikishwa kwa wananchi kupigiwa kura.” alisema.