Tunalaani mauaji ya wazee kwa imani za kishirikina

Mmoja wa vikongwe kijijini

Tangu jana tumekuwa tunaadika habari maalum kuhusu mauaji ya vikongwe mkoani Geita. Habari hiyo imejikita katika tukio la hivi karibuni kabisa la Mei 10, mwaka huu ambalo wanawake wanne, Esther Konya (55), Lolensia Bangili (70), Kulwa Mashana (65) na Rosa Masebu (65) waliuawa kinyama mno na kundi la wananchi wakiwatuhumu kwa ushirikina ambao ulisababisha fisi kumla mtoto wa miaka mitano, Diana Salu.

Habari hizi ni mfululizo wa kuitahadharisha jamii juu ya janga la wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kisingizo cha kukomesha ushirikina katika maeneo yao, lakini wakiacha kilio, chuki na simanzi isiyoelezeka kwa baadhi ya familia ambazo ndugu wao wanauawa bila kuwako kwa maelezo ya uhakika kuwa kweli ni wachawi, lakini baya zaidi bila kuwa wamepewa hata haki ya asili ya kusikilizwa kabla ya kuhukumiwa.

Kwa yeyote aliyesoma habari hizo jana na leo na tukiamini kwamba pia kesho atasoma mfululizo huo, atakubaliana nasi kuwa mauaji ya wanawake hawa wanaodaiwa kuwa ni wachawi ni janga la kijamii na kwa hakika hatua za haraka za kidola na kijamii zinahitajika kuchukuliwa ili kurekebisha hali hii.

Kwa mujibu wa binti wa mmoja wa wanawake waliouawa, mama yake katika kundi hilo alikuwa ndiye mwenye umri mdogo kupita wote, yaani miaka 55, ingawa umri huu ni wa kukadiriwa tu kukiwa na uwezekano wa kuwa chini ya hapo zaidi, siyo umri wa kuitwa kikongwe. Kwa maana hiyo, mauaji haya ingawa yanatajwa kuwa ni ya vikongwe, kimsingi yanalenga tu kundi la wanawake katika jamii kwa sababu nyingi tofauti.

Katika tukio la Geita la Mei 10, mwaka huu, habari zinasema kuwa chanzo ni mtoto wa miaka mitano kuliwa na fisi, lakini kwa kuwa akili za wananchi wa eneo hilo zinaamini tu kuwa kila kitu kinatokea kwa sababu ya kuwako kwa mkono wa mtu, walisadiki kuwa fisi aliyemla mtoto huyo anafungwa na kikongwe mmojawapo.

Hata hivyo, pamoja na juhudi za kumsaka fisi huyo katika nyumba ya kikongwe mmojawapo kutokuzaa matunda, hisia za kishirikina za wananchi hao hazikuwaruhusu kuwaza nje ushirikina na ulipizaji kisasi, hivyo walishia kuua wanawake wanne ambao sisi tunathubutu kusema kuwa hawakuwa na hatia kwa sababu hawakushitakiwa kwenye chombo chochote cha sheria, wakasililizwa, na kisha wakahukumiwa kwa mujibu wa sheria. Waliuawa kwa kuonewa tena kinyama mno chini ya kivuli cha msako wa wachawi.

Matukio ya mauaji ya vikongwe wanawake yamekuwa ni miaka na miaka katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora; hili ni tatizo la muda mrefu la kijamii; serikali kwa ujumla wake inajua na jamii pia inajua. Hakuna ushahidi wowote kuwa kweli wanaouawa ni wachawi, lakini baya zaidi haiyumkiniki kuwa katika jamii wachawi wawe ni wanawake tu, tena wazee.

Kumekuwako na juhudi za kutaka kukomesha hali hii, lakini kwa bahati mbaya hakuna mafanikio makubwa yaliyofikiwa ndiyo maana pamoja na elimu kutolewa kwa jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi katika kukabiliana na wahalifu wowote bila ya kuwafikisha kwenye vyombo vya sheia, bado tumeshuhudia wananchi wakiwaua wengine kwa visingizo ambavyo havina mashiko.

Ukisikia simulizi za binti ambaye alishuhudia mama yake akikatwakatwa mapanga mbele yake, utagundua kuwa katika utekelezaji wa ukatili huo kuna ulipizaji kisasi mwingi, kuoneana wivu kwingi, lakini zaidi kukomoana. Mambo haya yanafunikwa nyuma ya pazia, lakini mauaji yanafanywa kwa jina la kupiga vita ushirikina.

Tunasema bila kutafuna maneno, wote wanaoendesha mauaji haya ni watuhumiwa wa wahalifu, ni watu wanaostahili kufikishwa mahakamani kukabiliwa na kesi za mauaji kwa sababu moja kubwa, kwamba hakuna mwananchi mwenye mamlaka ya kumuhumu mwenzake kwa kesi yoyote bila kumfikisha mahakamani, achilia mbali kutekeleza hukumu kubwa kuliko zote ya kuodoa uhai wa wengine.

Tunalaani kwa nguvu zetu zote mauaji haya, tunataka jamii ikatae ujinga huu wa kupumbazwa na imani za kishirikina katika kuendesha maisha yao, watu wafunguke wasake elimu ili iwakomboe na kutambua mambo katika mantiki ya kisayansi.

Kwa kufanya hivyo tutaikomboa jamii dhidi ya janga la mauaji yanayofanywa chini ya mwavuli wa kusaka wachawi ilihali nyuma yake ni utekelezaji wa visasi, chuki, wivu na kila aina ya inda dhidi ya wengine. Jamii ni lazima sasa iamke na kutambua kuwa mauaji haya hayakubaliki na ni uhalifu kama uhalifu mwingine wowote.

CHANZO: NIPASHE