Na Joachim Mushi
MAKAMU Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto amesema tayari amewasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda kwa Spika wa Bunge, Anna Makinda.
Zitto amesema hayo alipokuwa akizungumza kwenye kituo kimoja cha redio jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumzia yaliyojiri katika vikao vya bunge lililopita ambalo wabunge wengi walionekana kuwa wakali dhidi ya utendaji wa baadhi ya mawaziri.
Katika mazungumzo hayo ambayo pia yalimshirikisha, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi, Nape Nnauye, Zitto alisema tayari amewasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kwa Spika Makinda-hoja ambayo alidai imeungwa mkono na wabunge 75 kutoka vyama mbalimbali vyenye wabunge bungeni.
Zitto alisema katika hoja hiyo wamemtaka Spika Makinda kuitisha Bunge la dharura ili wabunge wapate fursa ya kumuwajibisha Waziri Mkuu baada ya kushindwa kuwawajibisha mawaziri nane ambao wametanjwa kushindwa kutekeleza majukumu yao, na kusababisha ufujaji mkubwa wa fedha za wananchi.
Mawaziri wanaotajwa ni Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu, Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo, Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Mkuchika, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami na Naibu wake, Lazaro Nyalandu.
Hata hivyo alisema hoja yao itakufa tu endapo Serikali au Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete atawaondoa mawaziri hao katika baraza lake la mawaziri kwa kile kutuhumiwa kushindwa kulinda na kusimamia fedha na rasilimali za nchi kwenye vizara zao.
“Nasikitika sana mawaziri hao kuwa kimya hadi sasa…wajibu wetu (wabunge) ni kuishauri na kuisimamia Serikali, tumesha ishauri na sasa tunaisimamia. Kazi iliyobaki ni Rais Kikwete kuwawajibisha mawaziri hao,” alisema Zitto katika mazungumzo hayo.
Akizungumzia sakata hilo, Nape aliitaka Serikali kuwa makini na hoja na usahuri wa wabunge waliopaza sauti ya kutaka baadhi ya viongozi wanaoguswa katika tuhuma za matumzi mabaya ya fedha na usimamizi mbovu wa rasilimali za umma. Aliiomba serikali kuwa sikivu na kuchukua hatua mapema ili kurejesha heshima iliyopo chini ya uongozi wa Rais Kikwete.
“Tuwawajibishe wanasiasa lakini pia kuna haja ya kuangalia mfumo ambao viongozi hao wanafanyia kazi zao. Mfano Waziri Mkuu hana nguvu Kikatiba za kumvua uwaziri waziri moja kwa moja japokuwa yeye ndiye kiraja mkuu wa mawaziri wote…,” alisema Nape huku akisisitiza kuna haja ya kuangalia mfumo mzima wa utendaji serikalini.
Bunge lililomalizika limependekeza kuwajibishwa kwa mawaziri watano kutokana na ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) kuainisha upotevu mkubwa wa fedha za umma serikalini, baada ya kuzikagua wizara na idara anuai za Serikali.
Baada ya kuwasilishwa ripoti hiyo, wenyeviti wa kamati tatu; Hesabu za Mashirika ya Umma, Serikali za Mitaa na Serikali Kuu, nao waliwasha moto ambapo moja ya mapendekezo ya yao ni kuwajibishwa kwa mawaziri hao.
Wabunge wengi waliochangia taarifa hizo wakiwemo wa CCM waliwatuhumu mawaziri hao na baadaye Waziri Mkuu kuguswa kutokana na mamlaka yake kuwa ndiye Msimamizi Mkuu wa shughuli za Serikali bungeni.